1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Westerwelle azungumzia wasiwasi kuhusu Somalia

Josephat Nyiro Charo23 Julai 2010

Vita nchini Somalia vimekuwa mada muhimu katika ziara ya waziri Westerwelle, lakini hata hivyo Ujerumani haitaongeza juhudi zake nchini Somalia

https://p.dw.com/p/OTQs
Guido Westerwelle, waziri wa mambo ya nchi za kigeni wa UjerumaniPicha: Marcin Antosiewicz

Ziara ya waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, Guido Westerwelle, mjini Kampala, Uganda hapo jana imedhihirisha usuhuba uliopo kati ya nchi za Afrika na Ujerumani wakati kiongozi huyo alipokutana na mawaziri wa mashauri ya kigeni wa nchi hizo mjini humo.

Wakati alipotembezwa na naibu waziri wa mambo ya nchi za kigeni wa Uganda kwenye eneo kulikofanywa mashambulio ya mabomu mjini Kampala, waziri Westerwelle alionekana akiwa ameguswa sana na aliyoyaona na kuandika ujumbe wa katika kitabu cha rambirambi. Na wakati wa hotuba yake kwenye kikao cha mawaziri wa kigeni wa Umoja wa Afrika, bwana Westerwelle alizungumzia kuhusu mashambulio hayo na kutoa mwito kuwepo ushirikiano zaidi kuisadia Somalia.

"Ni lazima tushirikiane ili kuimarisha hali nchini Somalia. Ulaya inaliunga mkono bara la Afrika na inashirikiana nalo kuhakikisha kuna amani na usalama katika siku za usoni barani humo."

Ukweli lakini ni kwamba bwana Westerwelle hakubeba kwenye mkoba wake ahadi zozote za kuzipiga jeki juhudi za kupatikana ufumbuzi kwa mzozo wa Somalia. Wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani mjini Berlin hata hivyo imeahidi kuongeza msaada kwa Somlia kwa euro milioni 2,7 kwa ajili ya misaada ya kibinaadamu. Pesa hizo zitatolewa kwa shirika la msalaba mwekundu na zinapaswa kutumiwa kuwasaidia Wasomali waliojeruhiwa kwenye mapigano na waliolazimika kuyakimbia makazi yao kutokana na vita.

Mzozo wa Somalia unabakia vile ulivyokuwa. Umoja wa Afrika utatoa wanajeshi kwa ajili ya Somalia na Ujerumani na Umoja wa Ulaya zinabakia zikitazama kwa mbali. Kwa kuwa mazungumzo ya kutafuta suluhisho la kisiasa bado mpaka sasa hayajafua dafu, baadhi ya nchi wanachama katika Umoja wa Afrika zingependelea kupeleka wanajeshi zaidi nchini Somalia.

Yoweri Museveni
Rais wa Uganda, Yoweri MuseveniPicha: AP

Kabla mkutano wa kilele wa umoja huo mjini Kampala, rais wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni alipendekeza kupeleka wanajeshi 15,000 zaidi nchini Somalia. Waziri Guido Westerwelle analiona wazo hilo kuwa zuri lakini amesema, "Hilo ni swala ambalo sharti lijadiliwe na Umoja wa Afrika na singependa kulizungumzia kabla. Tunashukuru kwamba Uganda imejitolea kushiriki katika harakati nchini Somalia kwa sababu hiyo inaonyesha wajibu wa kanda nzima katika vita dhidi ya uharamia, jambo ambalo limejitokeza sana katika mkutano huu."

Swali kuu ni ikiwa kuongeza wanajeshi zaidi nchini Somalia kutasaidia kuutanzua mzozo uliodumu muda mrefu nchini humo. Tayari kuna wanajeshi 5,000 wa Umoja wa Afrika nchini Somalia ambao mpaka sasa hawajapata ufanisi mkubwa katika kuimarisha usalama na kudumisha amani nchini humo. Wanaudhibiti tu uwanja wa ndege wa Mogadishu, ikulu ya rais na kambi yao. Wasomali wengi hawawataki wanajeshi hao nchini mwao.

Waziri Westerwelle hakuzungumzia kuhusu changamoto hizo, bali alisisitiza mchango unaotolewa na Ujerumani nchini Somalia. Alikitembelea kituo cha mafunzo kwa ajili ya wanajeshi wa Somalia mjini Kampala, ambako wanajeshi wa Umoja wa Ulaya wanashughulika kuwapa mafunzo wanajeshi hao ambao hatimaye watatumwa Mogadishu kuisaidia serikali ya mpito ya Somalia kupambana na wanamgambo wa kiislamu. Ujerumani ina wanajeshi wake 13 wanaotoa mafunzo katika kituo hicho.

Waziri Westerwelle amerejea Ujerumani baada ya ziara yake iliyodumu muda wa takriban saa 18. Lakini kutokana na vitisho vya wanamgambo wa kiislamu kufanya mashambulio mapya, suala la Somalia linatarajiwa kuendelea kumtia tumbo joto waziri huyo.

Mwandishi: Josephat Charo/Pelz, Daniel / DW Afrika

Mhariri: Abdul-Rahman