1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Westerwelle kujaribu maripota wa Ujerumani waachiwe huru kutoka Iran.

Sekione Kitojo29 Desemba 2010

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wazungumzia kuhusu waandishi walioko kizuizini nchini Iran na usalama katika viwanja vya ndege.

https://p.dw.com/p/zr39
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Guido Westerwelle (FDP)Picha: dapd

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo wamezungumzia zaidi kuhusu waandishi habari ambao bado wako kizuizini nchini Iran, na hatua za udhibiti wa usalama katika viwanja vya ndege nchini Ujerumani.

Gazeti la Volksstimme la mjini Magdeburg likizungumzia kuhusu Wajerumani waliokamatwa nchini Iran , linaandika.

Kuhusiana na kukamatwa kwa maripota hao wa Ujerumani nchini Iran , waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, Guido Westerwelle anajikuta katika jukumu jingine jipya, akiwa kama mjomba mwema kutoka Berlin. Anaweza kufanikiwa kuwakomboa Wajerumani hao wawili ? Hilo analiushughulikia kiongozi huyo wa chama cha FDP muda mfupi kabla ya mkutano wake na viongozi wenzake wa chama hicho cha kiliberali. Kuachiliwa kwa haraka waandishi hao hakuonekani kuwa jambo linalowezekana. Wairan wamekubali kufanya mkutano wa siri , lakini hawafikirii kuwaachia huru kirahisi waandishi hao.

Gazeti la Süddeutsche Zeitung likizungumzia kuhusu mada hiyo linaandika:

Kama wanavyofanyiwa wafungwa wengine nchini Iran , ni lazima waandishi hao wa Ujerumani nao wafanyiwe hivyo hivyo. Baada ya wiki 11, ndugu wa maripota hao wameweza kuonana nao, na Wairan wanataka kuonyesha utu wa hali ya juu kwa wageni wao. Na hata kama maripota hao pamoja na familia zao watakapoagana na kwamba wamefurahi hata kama hawajaachiwa, ukarimu huu unaoonyeshwa ni kama mzaha. Na kile serikali ya Iran inachotaka kuonyesha ni uwezo wao, lakini sio utu. Kile ambacho wanaweza kuonyesha kama ukarimu ni kuwaachia waandishi hao.

Gazeti la Badische Neueste Nachrichten, kutoka mjini Karlsruhe linaandika kuhusu mada hiyo.

Ukweli ni kwamba lengo la kiadilifu , kwa waandishi habari ni kuikosoa Iran katika taarifa zao pamoja na kuelezea kukiukwa haki za binadamu nchini humo. Masuala hayo ni muhimu , wakati waandishi wanajaribu kufanya mahojiano na wakili wa mwanamke aliyehukumiwa kuuwawa kwa kupigwa mawe Sakineh Mohammadi-Aschtiani. Lakini ni muhimu pia kwa ajili ya kujikinga, kuheshimu sheria za nchi hiyo. lakini maripota hao , kuingia katika nchi hiyo kwa visa ya kitalii, ni ujinga.

Kuhusu hatua za usalama katika viwanja vya ndege nchini Ujerumani zilizochukuliwa kuanzia jana, ambapo wasafiri huwekwa katika makundi ambayo ni salama na yale ambayo huenda yakawa ni hatari kwa usalama, gazeti la Leipziger Volkszeitung linaadika.

Ni upuuzi tu, iwapo gaidi haonekani kama viongozi wa uwanja wa ndege wanavyofikiria. Kama hajavaa kama Bin Laden na amevalia kama mtu mwingine yeyote mwenye asili ya Ulaya. Iwapo ni mwanamke ama amevaa sare. Mpango wa kuwatenganisha watu sio tu ni wa kibaguzi, lakini pia unaleta hatari zaidi , kama udhibiti wa magaidi ulivyosababisha.

Nalo gazeti la Berliner Zeitung likizungumzia kuhusu mada hiyo linaandika:

Mtu anataraji kwamba mtu kama mkuu wa uwanja wa ndege wa Düsseldorf, Christoph Blume, ambaye hivi sasa ni kiongozi wa ngazi ya juu pia umoja wa viwanja vya ndege nchini Ujerumani, asingeweza kuanzisha mjadala wa kuchagua makundi ya wasafiri wenye kuleta kitisho. Baada ya pendekezo lake hilo, wasafiri watatengwa kulingana na, umri, jinsia, asili , uzoefu wa kusafiri mara kwa mara pamoja na vigezo vingine , na kisha kukabiliwa na udhibiti tofauti wa hali ya juu. Kwa maneno mengine vijana wa kiarabu wanaoonekana kama watu wazima , waliopata ruhsa ya kusafiri kwenda Marekani watafanyiwa uchunguzi maalum, wakati wanawake wa makamo wanaotoka Düsseldorf wakielekea Mallorca watapita bila taabu. Hii sio tu ni ujinga, lakini pia ni kinyume na katiba, ni uchunguzi bila kuwa na sababu maalum za tuhuma.

Ni maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani, kama mlivyokusanyiwa hii leo na Sekione Kitojo.

Mwandishi : Sekione Kitojo/ Inlandspresse.

Mhariri: Othman Miraj.