1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Westerwelle na Niebel wazuru Afrika pamoja

Josephat Nyiro Charo7 Aprili 2010

Badala ya kushindana wameamua kushirikiana

https://p.dw.com/p/MofP
Waziri wa nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle (kushoto) na waziri wa misaada ya maendeleo, Dirk NiebelPicha: AP/picture alliance/dpa/DW

Waziri wa nje wa Ujerumani Guido Westerwelle na waziri wa misaada ya maendeleo Dirk Niebel wanafunga leo safari ya bara la Afrika. Ziara hi ya kwanza kabisa ya pamoja ya mawaziri hao itakayomalizika Jumapili hii ijayo, inawachukua Tanzania, Afrika Kusini na Djibouti.

Kuvunjwa kabisa kwa wizara ya misaada ya maendeleo ambako kulidaiwa na chama cha kiliberali cha FDP kabla ya uchaguzi mkuu uliopita nchini Ujerumani, si suala tena linalozungumzwa. Kwa waziri wa misaada ya maendeleo Dir Niebel dai ni jibu lake kuwa wizara ya nje na ile ya misaada ya maendeleo mara nyingi, zimekuwa na mikakati tofauti. Lakini tangu uchaguzi mkuu uliopita, hali ya mambo imekuwa afadhali sana, amekuwa akisema tena na tena bwana Niebel. Akasema

"Haiwezekani kumuona waziri wa nje Jumatatu anafunga safari ya mji mkuu na waziri wa misaada ya maendeleo Alhamisi yake anafunga safari kwenda mji huo na kila mmoja anaeleza nyengine. Na hiyo, ndiyo sababu ya kutoa hoja ile, lakini sasa kwa vile tunahakikisha tunajitokeza kwa sauti moja katika siasa zetu za nje, kuwa na wizara mbili katika ushirikiano wa kimataifa bila ya shaka ni bora zaidi"

Leo mawaziri hao wawili hawakuhitaji kupanga kalenda zao, kwa vile wamefunga safari ya pamoja na ya kwanza nchi za nje hadi Afrika. Badala ya kushindana, wanaafikiana baina ya wizara zao - ndio azma ya waziri wa nje na mwanachama mwenzake wa chama cha kiliberali, FDP na ndio shabaha yao wanayotaka kuonesha katika safari hii ya pamoja.

Hali hii itanufaisha tu siasa ya nje kwa mujibu asemavyo bibi Marina Schuster, ambaye ni mbunge wa chama hicho cha FDP, anayetetea ushirikiano wa wizara hizo katika sera juu ya bara la Afrika. Anasema, "Tunataka kuonesha bara la Afrika liko sana moyoni mwetu na tunataka kwa pamoja kufahamu fursa zilizopo huko. Na hiyo ninavyoamini ni ishara muhimu kutoa."

Hasa katika suala la jinsi ya kulikabili bara la Afrika, kuna kasoro ya mfumo mmoja. Kwani kwa kuongezeka kwa fedha za misaada ya maendeleo kumechangia kuwa matawi mbalimbali tofauti yanapanga ushirikiano na nchi za kiafrika. Inatokea wakati mwingine mmoja hajui nini mwengine anafanya. Wakati wa serikali kuu ya muungano, kulikuwapo ukosefu wa ushirikiano kati ya wizara ya nje, afisi ya kansela na ile ya misaada ya maendeleo.

Ziara za waziri wa nje Westerwelle na waziri wa misaada ya maendeleo, Niebel nchini Tanzania, Afrika Kusini na Djobouti, zitafuata sasa mkondo huo wa siasa: kutoka Tanzania, mshirika wa kutegemea katika ushirikiano wa misaada ya maendeleo na Ujerumani, ziara yao itawachukua hadi Afrika Kusini. Afrika Kusini ndio gurudumu la uchumi la eneo la Afrika kusini mwa jangwa la Sahara na mshirika muhimu kwa viwanda vya Ujerumani, tena muda mfupi kabla ya firimbi kulia kwa kombe la dunia.

Hatua ya mwisho ya ziara yao fupi, itakuwa Djibouti huko pembe ya Afrika na hivyo watakuwa jirani kabisa na Somalia iliyosambaratika. Huko Somalia, tangu mwaka 2001, wamepelekwa wanamaji wa Kijerumani kupiga doria chini ya ile operesheni iliyopewa jina "Enduring Freedom". Wakati wa ziara hii, itabainika jinsi gani ushirikiano wa pamoja kati ya bwana Westerwelle na bwana Niebel ulivyo.

Mwandishi: Ute Schaeffer/ Ali Ramadhani/ZPR

Mhariri: Othman Miraji