1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO yaazimia kutokomeza ugonjwa wa kipindupindu ifikapo 2030

Sekione Kitojo
4 Oktoba 2017

Shirika la afya ulimwenguni WHO limeeleza matumaini yake ya kupunguza kwa kiasi kikubwa maambukizi ya ugonjwa wa kipundupindu  duniani na kupunguza idadi ya vifo vitokanavyo na ugonjwa huo kwa asilimia 90 ifikapo 2030.

https://p.dw.com/p/2lB3N
Krankenhaus von Bukavu RD Kongo Cholera  Afrika
Picha: DW/el Dorado

Hayo  yamesemwa  na  mkurugenzi anayehusika  na  masuala  ya  dharura katika  shirika  hilo Dr. Peter  Salama  alipokuwa  akizungumza  na  waandishi habari  mjini  Geneva.

Mkurugenzi  huyo  amesema  shirika  hilo  lingeweza kuchukua  hatua  za  haraka  na  kutuma  chanjo  zaidi  ili kupambana  na  ongezeko  kubwa  la  maambukizi  ya ugonjwa  wa  kipundupindu  nchini  Yemen  mwaka  huu.

Jemen Cholera-Ausbruch
Dawa za kupambana na ugonjwa wa kipindupindu nchini YemenPicha: Reuters/K. Abdullah

Dr. Peter Salama  bado  ameeleza  matumaini  yake kwamba , "tunakaribia  kufikia lengo," kuhusiana  na ugonjwa  huo  unaoweza  kuzuilika, unaosababishwa  na vijidudu  vilivyomo  katika  maji  ambao umefikia maambukizi  ya  watu  700,000  na  kusababisha  zaidi  ya vifo  vya  watu 2,000 mwaka  huu.

Lengo  ni moja  kati  ya  malengo  makubwa  ya  shirika  la WHO  kuutokomeza  kabisa  ugonjwa  huo  ama kupunguza  kwa  kiasi  kikubwa  ugonjwa  huo. Juhudi kama  hizo tayari  zipo  kwa  ugonjwa  wa  kupooza, malaria, surua, na  ukimwi. Hivi  sasa, ni ugonjwa  wa tetekuwanga  tu  ambao  umekwisha  tokomezwa katika uso  wa  dunia.

Jemen Cholera
Mgonjwa wa kipindupindu nchini YemenPicha: Picture alliance/Photoshot/M. Mohammed

India  na  nchi  zilizoko  katika  bara  la  Afrika  kusini  mwa jangwa  la  Sahara  zinakabiliwa  na  changamoto  ya muda  mrefu kupambana  na  kipindupindu.

Maeneo yanayozuka ugonjwa huo mara kwa mara

Maeneo  kama  Yemen  inayokabiliwa  na vita, ama Bangladesh, ambayo  imewapokea  zaidi  ya  wakimbizi 500,000  Waislamu  wa  Rohingya  kutoka  Mnyanmar, inakabiliwa  na  hali  ambayo  haitabiriki kwa  urahisi. Mpango  huo  wa  dunia  unalenga  katika  kupambana  na maeneo  yanayozuka  ugonjwa  huo   kila  mara , ambako kila  mwaka  katika  wakati  ule ule , ugonjwa  huo unazuka. Mpango  huo  unalenga  kuboresha  usafi  wa maji na  huduma  za  usafi , kwa  kutumia  chanjo za kunywa.

Somalia Hunger und Cholera fordern  mindestens 110 Todesopfer
Mlolongo wa akina mama wakisubiri kujipatia maji safi nchini SomaliaPicha: picture alliance/AP Photo/F. Abdi Warsameh

Mkakati  huo  unaweza  kusaidia  kutokometa  kipindupindu katika  mataifa  20  yaliyoathirika  ifikapo  mwaka  2030, kwa mujibu  wa  WHO. India  imeathirika  kwa  kiasi  kikubwa ikiwa  na  zaidi  ya  kesi  za  maambukizi 675,000 kila mwaka, kwa  mujibu  wa  shirika  la  WaterAid. 

Pia  ina idadi  kubwa  ya  watu  wanaoishi  bila  ya  kuwa  na uwezo  wa  kupata  maji  safi, na  salama , na  wengi wanaishi  bila  kuwa  na  vyoo sahihi.

Mosambik Cholera in Nampula
Maeneo ya mijini yakiwa na maji machafu ambayo yanaweza kuingia katika vyanzo vya maji na kusababisha magonjwa nchini MsumbijiPicha: DW/S. Lutexeque

Ethiopia  na  Nigeria , ambazo  zinafuatia  katika  nafasi  ya pili  na  tatu , pia  zina  idadi  ya  juu  ya  pili  na  ya  tatu ya  watu  wanaoishi  bila  maji  safi.

Mataifa  mengine  katika  nchi  kumi  za  juu ni  pamoja  na Haiti, Jamhuri  ya  Kidemokrasi  ya  Congo, Tanzania , Kenya , Bangladesh, Uganda  na  Msumbiji.

Mwandishi: Sekione Kitojo  / rtre

Mhariri: Iddi Ssessanga