1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO yaonya dhidi ya utaifa kuhusu chanjo ya COVID -19

Zainab Aziz
5 Septemba 2020

Mkurugenzi mkuu wa shirika la afya duniani WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus ametahadharisha juu ya kuifanya chanjo dhidi ya virusi vya corona kuwa suala la kitaifa.

https://p.dw.com/p/3i22o
Tedros Adhanom Ghebreyesus, Direktor WHO
Picha: picture-alliance/dpa/XinHua/Z. Cheng

Mkurugenzi huyo ametoa wito wa kupatikana kwa chanjo hiyo kwa njia ya haki. Kwa mujibu wa bwana Ghebreyesus nchi 78 zenye vipato vya juu zimejiunga na mpango wa kimataifa wa kupatikana kwa chanjo hiyo. Amesema mpaka sasa nchi 170 zimo katika mpango huo na idadi yao inaongezeka. Amezitaka nchi nyingine zijiunge hadi kufikia tarehe ya mwisho, Septemba 18.

Mkuu huyo wa shirika la afya duniani ameelekeza lawama za kificho kwa Marekani kutokana na nchi hiyo kujipatia mahitaji yake ya chanjo. Ghebreyesus amesema tiba inapaswa kutolewa kwa haki na kwa ufanisi. 

Chanjo salama na yenye ufanisi

Wakati huo huo Mkuu huyo wa Shirika la Afya Ulimwenguni amesema WHO haitapendekeza chanjo yoyote ya virusi vya corona kabla ya kuhakikisha kuwa ipo salama na yenye ufanisi. Tedros Adhanom Ghebreyesus alitoa maoni hayo mnamosiku ya Ijumaa, wakati ambapo Urusi na China tayari zimeanza kutumia chanjo zao za majaribio kabla ya utafiti wa muda mrefu kukamilika. Nchi zingine zimependekeza kurahisisha taratibu za kutoa idhini kwa ajili ya matumizi ya chanjo.

Mkurugenzi mkuu wa shirika la afya duniani WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema ana matumaini kuwa hivi karibuni kutakuwepo na chanjo ya kujikinga dhidi ya virusi vya corona inayofaa ili ulimwengu uweze kurudi katika hali ya kawaida.

Vyanzo:/RTRE/AFP