1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

William Hague amzungumzia Ntaganda

MjahidA26 Machi 2013

Wakati Bosco Ntaganda akitarajiwa kusomewa mashtaka yake katika mahakama ya ICC, waziri wa mashauri ya kigeni wa Uingereza, amesema hiyo ni hatua moja muhimu iliyopigwa kueleka mustakabali wa usalama mashariki mwa DRC

https://p.dw.com/p/184Fb
Waziri wa nchi za nje wa Uingereza Wiiliam Hague
Waziri wa nchi za nje wa Uingereza Wiiliam HaguePicha: AP

William Hague ambaye anafanya ziara kwenye eneo la maziwa makuu akiwa pamoja na mjumbe maalum wa shirika la umoja wa mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR Angelina Jolie, amesema hatua ya Bosco Ntaganda kupelekwa ICC na mwisho kufikishwa kizimbani ni moja ya mafanikio makubwa ambayo nchi za kikanda zimeweza kuyapata kwa kipindi kigumu cha usalama mdogo kwenye kanda ya maziwa makuu.

Hague amesema Rwanda imekuwa na mchango mkubwa kwenye mchakato huo ambao pengine unaweza kuiletea tija baadaye. "Hii ni moja ya mafanikio yaliyofikiwa na eneo zima, mathalan kukamatwa na kupelekwa Hague kwa Jenerali Bosco Ntaganda tunakaribisha maendeleo haya yote yaliyopatikana kwa kipindi kigumu. Lakini nisema tu kwamba Rwanda imekuwa na mchango mkubwa kwenye michakato hii yote." Alisema William Hague.

Mbabe wa kivita Bosco Ntaganda
Mbabe wa kivita Bosco NtagandaPicha: dapd

Msaada wa kigeni kukatizwa kwa Muda Rwanda

Uingereza ilikuwa miongoni mwa nchi za mwanzo kabisa kusitisha misaada yake kwa Rwanda mwezi November mwaka jana kufuatia ripoti ya wachunguzi wa umoja wa mataifa iliyoilaani Rwanda kulisaidia kundi la waasi wa M23 mashariki mwa DRC ambalo Bosco Ntaganda alikuwa mmoja wa viongozi wake wakuu.

Baadaye baadhi ya nchi za ulaya kama Ujerumani zilianza kurejesha misaada hiyo kwa madai kwamba nchi hiyo imeanza kuridhia matakwa ya wahisani. Pamoja na hayo lakini waziri wa mashauri ya kigeni wa Uingereza amesema hii haina maana kuwa Uingereza itaweza kuitoa misaada hiyo mara moja lakini kwa maoni yake akasema hii ni ishara njema kwa Rwanda na yumkini hatia hiyo ikafikiwa siku zijazo.

"Hakuna uamuzi wa haraka uliokwishachukuliwa juu ya hilo kwa miezi ya hivi karibuni.Kile ambacho tumekuwa tukikizungumzia ni sera na mienendo ya ushirikiano baina ya nchi mbili.Lakini bila shaka waziri wetu wa maendeleo ya kimataifa anaweza kulitathmini hilo kwa muda muafaka kwa kuzingatia tathmini ya jinsi sera hizo zinavyoheshimiwa. " Alisema william Hague

Waasi wa kundi la M23
Waasi wa kundi la M23Picha: Phil Moore/AFP/Getty Images

Kuondolewa kwa Ntaganda sio suluhu

Kwa upande mwingine baadhi ya wachambuzi wa siasa za maziwa makuu wanasema kuondolewa kwa Bosco Ntaganda kwenye mzozo wa DRC kunaweza kusilete suluhu la kudumu kwenye mzozo wa nchi hiyo.

Athanase Mbarushiki ambaye ni mchambuzi katika eneo hilo amesema kwa maoni yake Jenerali Ntaganda hakuwa chanzo cha tatizo katika eneo la maziwa makuu. Mbarushiki amesema kuna matatizo mengi ambayo hata hayatajwi na kama serikali ya DRC haitakuwa mstari wa mbele kuyatatua matatizo yake maana kuna makundi mengine kama ya kina Mudacumura na Nkunda na makundi mengine mengi haoni ni kwanini watu walimtazama tu Ntaganda.

Bosco Ntaganda aliyepelekwa ICC mwishoni mwa wiki iliyopita siku tano baada ya kujisalimisha kwenye ubalozi wa Marekani mjini Kigali anatazamiwa kufikishwa kizimbani kwa mara ya kwanza hii leo katika mahakama ya ICC mjini Hague Uholanzi kusomewa mashtaka yanayomkabili.

Mwandishi: Sylivanus Karemera/DW Kigali

Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman