Wimbledon: Lisicki asalim amri kwa Bartoli
7 Julai 2013Bartoli alipata ushindi wake wa kwanza wa Grand Slam siku ya Jumamosi wakati Mfaransa huyo alipofanikiwa kumshinda Sabine Lisicki kutoka Ujerumani kwa seti 2-0 , 6-1 na 6-4 katika fainali ya Wimbledon.
Bartoli mwenye umri wa miaka 28, ambaye alishindwa na Venus Williams katika fainali iliyopita ya Grand Slam ya Wimbledon mwaka 2007 , ni mwanamke wa tano mwenye umri mkubwa kiasi kuwa mshindi kwa mara ya kwanza wa mashindano makubwa.
Aendelea kutabasamu
Kwa upande wake Sabine Lisicki kama kawaida yake alikuwa akitabasamu huku akikiri kuwa alikuwa na wasi wasi mwingi kabla na wakati wa mchezo na kupoteza mchezo huo muhimu kwake na kwa Ujerumani kwa jumla.
Mjerumani huyo alionekana wazi kuwa fainali yake ya kwanza ya Wimbledon ilikuwa ngumu na alionekana dhahiri kuwa alikuwa anaelekea kupata kipigo cha kudhalilisha cha huenda 6-1 na 6-1. Lakini aliweza kupata ushindi katika michezo mitano mfululizo na kurejesha hali ya heshima .
Alibubujikwa na machozi uwanjani wakati akicheza seti ya pili na kujikuta akishindwa lakini alijikusanya upya kabla ya kuukabili umma wa mashabiki waliokusanyika uwanjani hapo na vyombo vya habari mbali mbali vya dunia.
Lisicki alimshinda bingwa mtetezi Serena Williams na makamu bingwa wa mwaka jana Agnieszka Radwanska katika njia yake kuelekea katika fainali, na alipigiwa upatu kumshinda Bartoli aliyeko katika nafasi ya 15 ya orodha ya wachezaji bora duniani.
Patashika nyingine
Leo Jumapili ( 07.07.2013) mashabiki wa mchezo wa tennis watarejea tena katika viwanja vya Wimbledon kushuhudia fainali ya wanaume, ambapo Novak Djokovic anapambana na Andy Murray katika fainali.
Kwa mara ya tatu katika Grand slam nne vijana hao wawili waliozaliwa karibu wakitofautiana kwa wiki moja watatiana kifuani kuwania taji hilo muhimu katika mchezo wa Tennis.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / afpe