1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wladmir Klitschko ampiga kumbo Chambers

22 Machi 2010

Hertha Berlin yawalaza mabingwa wolfsburg 5:1

https://p.dw.com/p/MZQO
Hertha Berlin wailaza Wolfsburg 5:1Picha: AP

Katika Bundesliga,Schalke, ilizuwiwa kuondoka na pointi zote 3 huko Hamburg pale Jonathan Pitroipa, alipoipatia Hamburg bao la kusawazisha 2:2.Katika Premier League,viongozi wa Ligi, Manchester United, walitoka nyuma na kuwapiga kumbo mahasimu wao wa jadi FC Liverpool kwa mabao 2:1.

Katika Ringi ya mabondia, Wladmir Klitschko wa Ukraine, amempiga kumbo sekunde 5 za mwisho,Eddie Chambers na kubakisha mataji yake ya WBO na IBF mjini Düsseldorf na mwimbaji mashuhuri Shakira, atatamba katika burdani maalumu mjini Soweto,Juni 10 katika mkesha wa kuanza Kombe la dunia nchini Afrika kusini-la kwanza barani Afrika.

Maajabu katika Bundesliga mwishoni mwa wiki-vigogo takriban vyote vilitiwa munda: Viongozi wa Ligi Bayern Munich, wazabwa mabao 2:1 na Eintracht Frankfurt; Bayer Leverkusen iliokua nafasi ya 3 yalazwa mabao 3:0 na Borussia Mönchengladbach na Schalke iliokuwa iunyakue usukani wa Ligi kutoka Bayern Munich iliondoka mwishoe sare 2:2 tu na hamburg.Kiroja kikubwa zaidi, timu iliopo mkiani mwa Ligi-Hertha Berlin, imewachezesha mabingwa VFL Wolfsburg, kindumbwe-ndumwe na kuwafedhehi numbani mwao kwa mabao 5:1.Hatahivyo, Bayern Munich, imesalia kileleni mwa Bundesliga licha ya pigo hilo la mabao 2:1 kutoka Frankfurt.

Kocha wao mdachi Van Gaal ,aliueleza mpambano wa Jumamosi hivi:

"Unaweza kusema kuwa Frankfurt ilistahiki ushindi.Lakini, sisi tulijichongea wenyewe kushindw ana hii yasikitisha."

Schalke, ikiongoza hadi dakika za mwisho huko hamburg kwa mabao 2:1 baada ya Kuranyi kutamba tena.lakini Mwishoe, Hamburg iliwaambia Schalke "kutangulia, si kufika." Kwa mabao 2:2, Schalke ilinyimwa na Hamburg nafasi ya kuongoza Bundesliga na kuiacha nyuma Bayern Munich.

Maajabu pia yalipita mkiani mwa Bundesliga,kwani, timu ya mkiani kabisa imeiangusha ile ya juu kabisa: Hertha Berlin, inayouburura mkia wa Ligi na iko hatarini kuteremshwa daraja ya pili, iliwafedhehesha jana mabingwa VFL Wolfsburg kwa mabao 5:1.Kocha wa Berlin,alieitwa kuiokoa timu ya jiji kuu akivuta pumzi alisema,

"Leo tumeweza kucheza makini kabisa na kila mmoja ameona ,jinsi timu iliopo mkiani mwa ngazi ya ligi ilivyoweza kutamba."

Ama katika Premier League, Manchester United ilitoka nyuma na kuwakandika mahasimu wao wa jadi FC Liverpool ,mabao 2:1 ili kubakia kileleni.Kwanza lakini, alikua Fernando Torres,alielifumania lango la Manu ,lakini haukupita muda, jogoo la Manu, wayne Rooney,likajibu.

Mkorea Kusini, Park Ji-sung, nae akatia bao la ushindi kwa Manchester United .Ushindi wa Manu na kuteleza kwa Chelsea, kumeifanya Manu kuongoza Premier League kwa pointi 2 kutoka ilipo Arsenal ,ilioishinda West Ham mabao 2-0.

Chelsea,imeangukia pointi 2 nyuma ya Arsenal kwa kumudu sare yabao 1:1 na Blackburn.Chelsea lakini wana mpambano 1 hawakucheza.

Katika la Liga-ligi ya Spain,"mchezaji bora wa dimba wa mwaka wa ulaya na dunia" , Lionel Messi,alitia mabao 3 -hattrick- katika ushindi wa mabao 4:2 kwa Real zaragoza.Barcelona iko sasa pointi sawa na Real madrid iliotoka nyuma na kuitandika Sporting Gijon mabao 3-1.Hatahivyo, Real inaongoza ligi ya Spain kwa wingi wa magoli.

Kombe la dunia la FIFA likikaribia hapo Juni 11 mwaka huu pale wenyeji Afrika Kusini watakapo fungua dimba Juni 11 na Mexico, usiku wa Juni 10,kuamkia mpambano huo, burdani kubwa itafanyika mjini Soweto.

Stadi mkubwa ataketamba si mwengine bali Shakira.Burdani hiyo itakayofanyika katika uwanja unaochukua mashabiki 30.000 mjini Johnnesberg.

Miongoni mwa burdani nyenginezo ,wacheza ngoma wa kiafrika na wanamuziki kama vile mzaliwa wa Benin, Angelique Kidjo.Amadou na Mariam kutoka Mali,kikundi cha muziki cha Afrika kusini "Parlotones" ni miongoni mwa vikundi vitakavyo tumbuiza.

Timu ya Taifa ya wasichana ya Tanzania-Twiga Stars,inajiwinda sasa kwa changamoto na Eritrea baada ya kuilaza Ethiopia.Twiga Stars inaania kushiriki katika Kombe la Afrika la wanawake nchini Afrika kusini.

Tumalizie katika ringi ya mabondia:

Mbabe wa wezani wa juu ulimwenguni kutoka Ukraine, Wladmir Klitschko, alitetea mataji yake 2 ya WBO na IBF usiku wa Jumamosi alipofaulu sekunde 5 za mwisho za duru ya 12 na ya mwisho kumpiga kumbo (knock-out) Eddie Chambers wa Marekani. Ikionekana kana kwamba, mbabe Klitschko angeshinda kwa pointi,sekunde 5 za mwisho, alimvurumishia Chambers konde kali la ghafula lililomtoa nje ya ndoto zake za kuvaa taji la dunia.

Mwandishi: Ramadhan Ali /RTRE

Mhariri: Abdul-Rahman,Mohammed