1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Xi amuapisha kiongozi mpya Hong Kong

Sekione Kitojo
1 Julai 2017

Rais wa China Xi Jinping amemuapisha kiongozi mpya wa Hong Kong leo Jumamosi (01.07.17)huku akionya China haitavumilia changamoto yoyote dhidi ya mamlaka yake.

https://p.dw.com/p/2fkEv
China Carrie Lam und Präsident Xi Jinping in Hongkong
Picha: Reuters/B. Yip

Hayo  ameyasema katika hotuba  yake yenye maneno makali kuadhimisha miaka 20 ya koloni hilo la zamani la  Uingereza kurejea kwa China. Usalaama uliimarishwa katika eneo  la  bandari  ambayo miongo miwili  iliyopita , gavana  wa  zamani  wa  kikoloni , Chris Patten , akimiminikwa  na  machozi  aliikabidhi  Hong Kong kwa  China  katika sherehe  ambayo  ilifanyika  huku  mvua  kubwa ikinyesha.

China Carrie Lam in Hongkong
Kiongozi mpya wa Hong Kong Carrie LamPicha: Reuters/B. Yip

"Jaribio  lolote la  kuhatarisha  uhuru   na  mipaka  ya  China pamoja na  usalama  wake, ni  sawa  na  kupambana  na  dola ya  serikali kuu  ya  China  na  mamlaka  ya sheria mama  ya  HKSAR ama kuitumia  Hong Kong  kuingilia  na  kuvuruga  shughuli  dhidi  ya China  bara  katika  hatua  ambayo inavuka  mstari  mwekundu  na haitakubalika  kabisa," amesema  Xi.

Chini  ya  katiba  ndogo  ya  Hong Kong , sheria  ya  msingi, jimbo hilo  ambalo  ni  sehemu  muhimu  ya  kiuchumi  inahakikishiwa uhuru wake kwa "takriban miaka  50" baada  ya  mwaka  1997. HKSAR ina  maana  ya  jimbo  maalum  la  utawala  la  Hong Kong, ambalo  linaongozwa  chini  ya  utaratibu  wa  "nchi  moja , mifumo miwili" unaoruhusu  mamlaka  makubwa  ya  ndani.

Maneno  ya  Xi  ni  makali  kuwahi  kutolewa  kwa  eneo  hilo la  kituo cha masuala  ya  fedha  duniani na  yanakuja  katika  wakati  wa wasi  wasi  mkubwa  wa  kijamii  na  kisiasa  na  yanajumuisha  kile ambacho  wengi  katika  jimbo  hilo  la  Hong Kong  wanaona  ni  hali inayoongezeka  ya  kuingiliwa  na  serikali  kuu  ya  China   katika masuala  ya  ndani  ya  mji  huo.

China Vereidigung in Hongkong
Wajumbe wa baraza kuu la utawala wa Hong Kong wakila kiapoPicha: picture-alliance/ZUMA Wire/Xinhua/Li Tao

Alikuwa  akihutubia  ukumbi  uliojaa  wageni  waalikwa  pamoja  na watu  mashuhuri  wengi  wao  wakiwa  ni  waungaji  mkono  serikali kuu  mjini  Beijing , akizungumza  kwa  zaidi  ya  dakika  30 , baada ya  kumuapisha  kiongozi  wa  kwanza  mwanamke  wa  Hong Kong, Carrie Lam.

Ghasia za hapa na pale

Vurugu  za  hapa  na  pale  zilitokea  nje  ya ukumbi  huo  wakati wanaharakati  wanaodai  demokrasia  zaidi , baadhi  wakiwa  na mabango  yenye  maneno "demokrasia. Utawala  wa  ndani," na makundi  yanayopendelea  China  walitupiana  maneno, huku  mamia ya  polisi  wakiwekwa  katika  siku  hii  ya  kihistoria  ya maandamano  mjini  Hong Kong.

Waandamanaji  kadhaa  wanaodai  demokrasi  walichukuliwa  na polisi , wakati makundi  kadhaa  yanayounga  mkono  serikali  ya China , yakishangilia  kwa  nguvu  na  wakipunga  bendera  kama vile  kwa  kuonesha  ushindi.

China Präsident Xi Jinping und seine Frau Peng Liyuan kommen am Flughafen in Hongkong an
Rais Xi akiwasili katika uwanja wa ndege pamoja na mkewePicha: Reuters/B. Yip

Rais Xi Jinping  alisema  Hong Kong  ni  huru  zaidi  kuliko ilivyokuwa  hapo  kabla  lakini  akaonya  dhidi  ya kile  alichosema "changamoto ambazo  zisizoruhusika" dhidi  ya  mamlaka  ya  Beijing.

Lam alichaguliwa  na  kamati  inayounga  mkono China , kama walivyo  watangulizi  wake, na  tayari  anaonekana  na  wakosoaji kuwa  ni  kibaraka  wa  China  katika  mji  ambako  wengi wamekasirishwa  na  China  inavyoongeza mbinyo  dhidi  ya  uhuru wa  watu  karibu  milioni nane.

Lam alikula  kiapo  kuingia  madarakani  chini  ya  bendera  ya  taifa la  China  katika  kituo  cha  makutano  katika  bandari  mjini  Hong Kong, kabla  ya  kushikana  mikono  na  Xi.

China pro-Demokratie-Proteste Hongkong
Maandamano ya watu wanaopendelea China mjini Hong Kong wakipambana na wanaopinga mjini Hong Kong - 01.07.2017Picha: picture-alliance/AP Photo/Ng Han Guan

Kuapishwa  kwake  kunakuja  siku moja  baada  ya  wizara  ya mambo  ya  kigeni  ya  Beijing  kutangaza  kwamba  waraka  uliotiwa saini na  Uingereza  na  China  ambao  ulisababisha  mji  huo kukabidhiwa  China kwamba "hauna  maana  tena".

Mwandishi: Sekione  Kitojo / afpe / rtre

Mhariri: Sylvia  Mwehozi