1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Xi Jinping ataka kuirudisha nyuma China

Oumilkheir Hamidou
27 Februari 2018

Xi Jinping na kiu cha kung'ang'ania madaraka nchini China, hali nchini Syria na mkutano mkuu wa dharura wa chama cha Christian Democratic Union CDU ni miongoni mwa mada magazetini .

https://p.dw.com/p/2tORG
China 2007 Xi Jinping, Kommunistische Partei Shanghai
Picha: picture-alliance/dpa/E. Wang

Tunaanzia  jamhuri ya umma wa China ambako rais Xi Jinping anaonyesha kuigiza ule usemi wa kiswahili "Mramba asali harambi mara moja!" Anasemekana ana azma ya kutaka kupindukia mihula miwili madarakani. Gazeti la "Leipziger Volkszeitung" linaandika : "Xi Jingping aliwahi mwenyewe kusema, madaraka mahala pake ni ndani ya tundu. Alikusudia wakati ule maafisa wa chama chake waliokuwa wakijitajirisha bila ya kutahayari. Sasa Xi anaonyesha matamshi hayo sio tu yanamhusu  yeye mwenyewe  bali anaielekeza China katika zile enzi za utawala wa mabwanyenye, na hajali lawama kutoka nje sikwambii  tena kutoka ndani. Anahoji uongozi wake ni muhimu kwa utulivu wa nchi hiyo na kuimarisha mfumo wa kijamaa. Yote hayo tumewahi wakati mmoja kuyasikia. Utawala wa kiimla unaanzia pale ambapo kiongozi pekee aliyeko madarakani anashindwa kuvumilia majibishano. Kwa bahati mbaya historia inadhihirisha watawala kama hao hawawezi tena kung'olewa madarakani bila ya damu kumwagika."

Rais Putin aamua silaha ziwekwe chini katika jahanam ya Ghouta Mashariki

Maoni sawa na hayo yameandikwa pia na mhariri wa gazeti la  "Hannoversche Allgemeine" anasema Xi Jinping anataka kuirejesha nyuma jamhuri ya umma wa China. Hali nchini Syria pia imemulikwa magazetini hii leo. Na gazeti la "Der Tagesspiegel", linazungumzia makubaliano ya kuweka chini silaha na kuandika: "Saa tano kwa siku, jahanam ya Ghouta ya Mashariki inatakiwa itulie. Uamuzi huo umepitishwa na rais wa Urusi Vladimir Putin aliyewaamuru wanajeshi wake waheshimu mpango wa kuweka chini silaha. Si suala la kuwaonea watu huruma hilo. Ingekuwa hivyo basi Putin angeingilia kati tangu zamani na kumzuwia muimla wa Syria. Hayo lakini kiongozi wa Kremlin hakuyafanya. Kuna ripoti za kuaminika zinazosema kwamba ndege za kivita za Urusi pia zimeshiriki katika kuihujumu ngome ya waasi karibu na Damascus. Kabla ya uchaguzi wa rais nchini Urusi, Marchi 18 inayokuja, labda Putin anataka kwanza kutangaza ushindi wa kijeshi nchini Syria. Kwa hivyo amri hiyo ya kuweka chini silaha si chochote chengine isipokuwa mbinu tena ya kuchukiza. Masaa matano bila ya risasi, na baadae zifyetuliwe upya."

Angela Merkel imara kileleni mwa CDU

 Mada yetu ya mwisho magazetini inatupeleka mjini Berlin ambako chama cha Christian Democratic Union-CDU kimeidhinisha makubaliano ya kuunda serikali ya muungano pamoja na SPD kwa wingi mkubwa. Gazeti la "Trierische Volksfreund" linaandika:" CDU wamedhhirisha jinsi walivyo. Waangalifu na mijadala inapozuka hawakawii kutuliza hali ya mambo. Upungufu wa asili mia nane katika uchaguzi mkuu uliopita, hawana wizara ya fedha, yote hayo hayakupewa umuhimu mkubwa katika mkutano mkuu wa dharura mjini Berlin. Angela Merkel, hata baada ya miaka 18 ya ungozi wa chama hicho, bado ana uwezo , ikilazimika, kutambua hali namna ilivyo na kupitisha maamuzi yanayohitajika. Kwa wakati huu tulio nao tunaweza kusema vyama ndugu vya CDU/CSU ndio pekee wenye kiu cha kuongoza nchi wakati huu tulio nao."

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri:Yusuf Saumu