1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yaliyochambuliwa na wahariri wa Ujerumani

Oummilkheir7 Desemba 2006

Ripoti ya Baker na kitisho cha matumizi ya nguvu katika shule za Baden-Württemberg ndizo mada zilizomulikwa magazetini hii leo

https://p.dw.com/p/CHUG

Ripoti ya tume ya Baker kuhusu Irak na msako wa polisi katika shule kadhaa za jimbo la Baden-Württemberg,baada ya onyo, kupitia mtandao wa Internet ,huenda pakazuka balaa kama lile lililoshuhudiwa wiki mbili zilizopita mjini Emsdetten,ndizo mada zilizopewa umbele na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo.

Walihitaji muda mrefu kutathimini hali ya mambo,na sasa wataalam hao wanaoongozwa na waziri wa zamani wa mambo ya nchi za nje wa Marekani James Baker wametangaza ripoti yao kuhusu sera za Marekani kuelekea Irak.Tume ya Baker inaisihi serikali ya Marekani irejee katika njia ya diplomasia ili kuitoa Irak katika hali ya vurugu na kufungua njia ya kuwarejesha nyumbani haraka wanajeshi wao.Na ili amani iweze kupatikana tume ya Baker inaishauri Marekani izungumze na Syria na Iran.Gazeti la mjini Bonn,GENERAL-ANZEIGER linahisi:

“Wahafidhina mambo leo mjini Washington wanatambua fika kwamba wameshindwa . Baker ameangukiwa na jukumu tuu la kutangaza hadharani .Kurejeshwa nyumbani wanajeshi si siri tena.Lakini suala hapa ni jee warejee kwa kila hali?Hata ikiwa nchi hiyo itatumbukia katika janga la vita vya wenyewe kwa wenyewe?Ikiwa Iran,Saud Arabia na Uturuki zitautumia mwanya ulioko na kuunga mkono jamii na waumini wa madhehebu yao nchini Irak?Licha ya maoni jumla yaliyoko nchini Marekani,vita hivi vikome haraka iwezekanavyo,kimoja ni dhahiri,hakuna anaetaka kuiacha Irak itumbukie katika janga la mtafaruku.”

Gazeti la Berliner Zeitung linaamini rais Bush atabadilisha mkondo wa siasa yake.Gazeti linaandika:

“Kila kitu kinaonyesha kwamba Bush atalazimika kuzingatia hoja za wenye misimamo ya busara katika siasa za Marekani.Kwa hivyo hata mazungumzo yatafanyika pamoja na serikali za Iran na Syria.Watabidi pengine kuzungumza pia na Hamas na Hisbollah.Yote hayo yanatoa ishara ya matumaini mema,sio pengine kwa masilahi ya siasa ya nje iliyoshindwa ya Marekani,lakini kwa wananchi husika nchini Irak na mashariki ya kati.”

Gazeti la Frankfurter Allgemeine Zeitung linashuku kama kweli rais wa Marekani yuko tayari kujifunza.Gazeti linaandika:

“Kamisheni isingepata njia nyengine bora ya kujitoa kifua mbele kuliko hii.Lakini hilo sio suala watu wanalojiuliza.Kilichoingia midomoni ni kama njia hiyo itafuatwa.Watu wanapata shida kuamini kama rais huyu ambae kila kitu amekua akikiulia masikio,atakubali kweli safari hii kusikiliza yasemwayo.Akibadilisha mkondo wa mambo,itamaanisha mabadiliko yatakawia kutekelezwa.”

Na hatimae gazeti la NEUE WESTFÄLISCHE la mjini Bielefeld linahoji:

„Zaidi ya wanajeshi elfu tatu wa Marekani wameuwawa nchini Irak, hadhi ya shirika la upelelezi la CIA imechujuka,Sifa za Marekani kama nchi inayofuata sheria zinawekewa alama ya kuuliza,eneo zima la mashariki linakumbwa na mtafaruku,na raia wasiokua na idadi wamebidi kupoteza maisha yao hadi Washington ilipokuja kutanabahi:Hatuwezi kushinda nchini Irak.Imekwenda kwendaje hata rais akapotea njia kama hivyo.Bush aliamini akiendesha vita dhidi ya rafiki wa magaidi na muimla Saddam Hussein,angefanikiwa mara dufu:kuwavunja nguvu magaidi na kuwakomboa wanaodhulumiwa.Wanasiasa wanaposhindwa kama hivi,kawaida wangebidi kujiuzulu.“

Tuigeukie mada ya pili magazetini.Shule kadhaa za jimbo la Baden-Württemberg zilikaguliwa na polisi jana,baada ya mwanafunzi mmoja kuandika kupitia mtandao wa Internet,anapanga kuivamia shule moja ya jimbo hilo.

Japo kama lilisalia kua tishio tuu,lakini kisa kama hicho kilichosababishwa damu kumwagika wiki mbili zilizopita huko Emsdetten ,bado kiko vichwani mwa watu na mjadala umeenea vipi kuzuwia matumizi ya nguvu shuleni.