1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yanayojiri kwenye mvutano wa kisiasa wa nchini Uhispania

Zainab Aziz
30 Oktoba 2017

Wafanyakazi wa serikali leo hii Jumatatu wameanza wiki ya kazi tangu serikali kuu ya Uhispania ilipobatilisha tamko la uhuru wa jimbo la Catalonia kwa kumvua madaraka kiongozi wa jimbo la hilo Carles Puigdemont.

https://p.dw.com/p/2mjMY
Spanien - Demonstrationen für die Einheit von Spanien und Katalonien in Barcelona
Picha: Reuters/Y. Herman

Wafanyakazi wa serikali walipofika mahala pao pa kazi leo hii wamekuta bendera zote mbili za Uhispania na jimbo la Catalonia zikipepea juu ya majengo ya serikali. Bila shaka kinachosubiriwa kwa shauku ni iwapo hali ya utulivu itaendelea kuzingatiwa wakati serikali kuu ya Uhispania inapotekeleza hatua ya kuchukua mamlaka ya jimbo hilo? hata ingawa hali hiyo inadhaniwa kuwa inaweza ikazusha mvutano zaidi katika nchi ambayo imekumbwa na mgogoro wa kisiasa kwa muda wa mwezi mmoja sasa. Wakati huo maelfu ya watu wanaounga mkono Catalonia kubakia katika Uhispania moja walifanya maandamano makubwa katika mji wa Barcelona.

Spanien Katalonien Rede Carles Puigdemont
Kiongozi wa jimbo la Catalonia aliyevuliwa mamlaka Carles PuigdemontPicha: picture-alliance/AP Photo/Presidency Press Service

Hakuna ishara yoyote iwapo baraza la mawaziri wa jimbo la Catalonia lililoondolewa madarakani  litajaribu kurejea kwenye ofisi zao siku ya Jumatatu baada ya baraza hilo kushiriki katika kura ya siri juu ya jimbo la Catalonia kujitenga na Uhispania mnamo siku ya Ijumaa.  Kiongozi wa Catalonia Carel Puigdemont amesema ataendeleza upinzani kwa kutumia njia za kidemokrasia dhidi ya hatua zilizochukuliwa na serikali kuu za kuyatwaa mamlaka ya jimbo lake kwa kuahinisha ibara ya 155 ya katiba ya Uhispania. Hata hivyo tamko hilo la Puigdemont halikufafanua kama linamaanisha ndio amekubali uchaguzi wa mapema ufanyike kama hatua mojawapo ya kupunguza mvutano baina ya jimbo lake na serikali kuu ya mjini Madrid. Kiongozi huyo wa Catalonia anaweza kuingia kwenye lawama nzito leo hii za uhaini na kuvuruga uchumi. Waziri wa mambo ya nje wa Uhispania Alfonso Dastis amesema ana imani kuwa serikali kuu itarejesha hali ya utulivu na sheria katika jimbo la Catalonia. Dasdis amesema serikali kuu ina imani kuwa mpaka sasa ukweli umedhihirika na kwamba busara itarudi kwenye mawazo ya Wacatalonia ili kjuweza kutambua kwamba kiongozi wa zamani wa jimbo la Catalonia alitoa ahadi za uongo.

Kiongozi wa Catalonia aliyenyang‘anywa mamlaka Carles Puigdemont amechapisha ujumbe ulioandamana na picha kwenye mtandao wa kijamii, picha hiyo inamwonyesha akiwa amekaa kwenye ua wa bunge katika jimbo la Barcelona. Picha hiyo imeambatanishwa na ujumbe wa maandishi yasemayo ''Habari za Asubuhi'' pamoja  na kikaragosi kinachotabasamu. Picha hiyo imezua maswali mengi iwapo Puigdemont yuko ndani ya majengo ya bunge?

Serikali kuu ya Uhispania inayoongozwa na Waziri Mkuu Mariano Rajoy moja kwa moja itasimamia mamlaka ya jimbo la Catalonia. Serikali kuu ya Uhispania tayari imeshatwaa udhibiti wa jeshi la polisi katika jimbo hilo, imelivunja bunge na imeitisha uchaguzi wa mapema utakaofanyika tarehe 21 mwezi Desemba.

Mwandishi:Zainab Aziz/AFPE/APE

Mhariri:   Mohammed Abdul-Rahman