1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yar'Adua arejea Nigeria

25 Februari 2010

Rais Umaru Yar'Adua wa Nigeria aliwasili mjini Abuja usiku wa kuamkia leo, miezi mitatu tangu alipoondoka nchini humo kuelekea Saudia Arabia kwa matibabu.

https://p.dw.com/p/M9fw
Rais Umaru Yar'Adua arejea NigeriaPicha: AP

Ndege iliyombeba Yar'Adua ilitua katika eneo maalum lililotengewa ndege ya Rais katika uwanja wa ndege wa Abuja, huku kukiwa na ulinzi mkali. Vyanzo vya habari vinasema Yar'Adua aliondoka mjini Jeddah saa nne za usiku hapo jana. Hakuna taarifa yeyote imetolewa hadi sasa kuhusiana na hali ya afya ya Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 58, anayeugua maradhi ya moyo na figo.

Ingawa serikali haikutoa taarifa yeyote kuashirikia kuwa Rais Yar'Adua anarejea nchini Nigeria- uwanja wa ndege mjini Abuja ulikuwa chini ya ulinzi mkali, huku maafisa wa usalama na wanajeshi wakishika doria katika barabara za kuelekeea katika makao rasmi ya ya Rais.

Nigeria Jonathan Goodluck
Makamu wa Rais Jonathan Goodluck anahudumu kama Rais wa muda.Picha: AP

Na kama mtu yeyote anavyoelewa siasa za Nigeria hii ilikuwa ishara tosha mgeni mashuhuri katika uwanja huo si mwingine bali ni Rais Yar'Adua. Gari la Ambulansi na magari mengine ya kifahari yaliwasili katika uwanja wa ndege wa Abuja usiku wa manane saa kadhaa baada ya vyanzo vya habari kuripoti kuwa Rais Yar'Adua ameondoka Jeddah, akiwa njiani kurejea nchini Nigeria.

Waandishi wa habari walizuiwa kufika katika eneo hilo maalum la Rais katika uwanja huo wa ndege. Msafara wa gari 23, ikiwemo Ambulansi ambazo zikiwa na ulinzi mzima wa Kirais baadaye uliondoka katika uwanja huo wa ndege ukielekea katika makao rasmi ya Rais.

Hakuna taarifa zozote ambazo zimetolewa hadi kufikia sasa kuhusiana na afya ya Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 58, na pia haijulikani kama Yar'Adua anaweza kuendelea kutawala au iwapo Makamu wa Rais Goodluck Jonathan ataendelea kuhudumu kama rais wa muda.

Nigeria Unruhen Militär bei Jos
Nigeria ina historia ya mapinduzi ya kijeshi.Picha: AP

Kutokuwepo kwa Yar'Adua nchini Nigeria nusura kuitumbikize nchi hiyo katika mzozo wa kikatiba na kutishia kukwamisha operesheni zote za serikali. Hili lilitawatuliwa wiki mbili zilizopita pale Makamu wa Rais Goodluck alipoapishwa kama Rais wa muda.

Tangu hapo Jonathan ameuvalia njuga wadhifa kamili wa rais, akifanya mabadiliko katika baraza la mawaziri, akiahidi kupambana na ukosefu wa kila mara wa umeme nchini humo, na pia kuendeleza juhudi za mapatano katika eneo lenye utajiri wa mafuta Niger Delta.

Baadhi ya wanasiasa wamesema huenda Jonathan akaweza kupata kuungwa mkono kugombea urais katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Aprili mwaka ujao. Kuwasili kwa Yar'Adua bila shaka kunazua wasiwasi hasa miongoni mwa wanasiasa, ambao wengi wanasemekana walikuwa wameanza kujitayarisha, Nigeria bila ya Yar'Adua.

Baraza la mawaziri ambalo mara mbili limepitisha azimio kusema hakuna sababu yeyote ya kutangaza kuwa rais Yar'Adua hawezi tena kutawala, linatazamiwa kukutana tena baadaye leo.

Umaru Yar'Adua amekuwa akiugua ugonjwa wa moyo, huku madaktari wakisema eneo linalohifadhia moyo wake limeathirika. Mwezi Novemba mwaka uliopita, Yar'Adua alisafirishwa hadi hospitali ya Mfalme Faisal huko Jeddah kutibiwa. Yar'Adua ambaye pia ana historia ya maradhi ya figo hajaonekana hadharani tangu hapo Novemba.

Mwandishi: Munira Muhammad/ AFPE

Mhariri: Abdu Mtullya.