1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yemen hali bado ni tete.

Admin.WagnerD20 Aprili 2015

Makamanda wa kijeshi wa mkoa mmoja mkubwa nchini Yemen wametangaza utiifu wao kwa Rais Abu Rabbu Mansur Hadi aliye uhamishoni wakati huu nchini Saudi Arabia.

https://p.dw.com/p/1FBHU
Jemen Saudi-Arabien Luftangriff auf Sanaa
mashambulizi ya Saudia yaharibu zana za WahouthiPicha: Reuters/N. Quaiti

Katika kile kinachoonekana kama ni kumuunga mkonno Rais Mansur Hadi na serikali yake, Viongozi wa kijeshi wa kikosi cha wanajeshi 25,000 katika mkoa mkubwa kabisa nchini Yemen wamesema wako nyuma ya kiongozi huyo. Taarifa ya maafisa wa kijeshi na wanajeshi wa kikosi hicho kilichoko Hadramawit, ilitolewa na Meja Jenerali Abdelrahman Al-Halili. Kwa upande mwengine wanamgambo wa Kishia wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran wanaendelea kuyadhibiti maeneo makubwa ya Yemen ukiwemo mji mkuu sanaa, huku mapigano na majeshi yanayoiunga mkono serikali nayo yakiendelea.

Ndege za muungano wa kiijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia zimefanya mashambulizi kwenye kituo kimoja cha makombora cha kikosi cha ulinzi wa rais wa zamani Ali Abdullah Saleh katika milima ya Fajj Attan kusini mwa Sanaa, na kusababisha miripuko mikubwa ilioyatikisa majengo kadhaa ya mji mkuu. Abdullah saleh ni mshirika wa Wahouthi katika vita hivyo. Taarifa zinasema mapigano yalioanza alfajiri ya leo pia yamewauwa kiasi ya Wahouthi 21 katika miji ya Dahleh na Huta, wakati msemaji wa muungano huo wa kijeshi Nrigedia Ahmed Al-Assiri akisema tayari wameshafanya mashambulizi ya anga 2,000 tangu operesheni hiyo ianze. Shahidi mmoja alisema hospitali katika eneo hilo imejaa majeruhi na kelele za maumivu, ya majeraha yaliosababishwa na maporomo ya nyumba zao.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Yemen Riyadh Yassin leo amelikataa pendekezo la Iran kuwa tayari kuwa msuluhishi wa mgogoro huo akisisitiza kwamba Iran inawaunga mkono waasi wa Houthi. Akizungumza katika kandoni mwa mkutano wa kiuchumi wa nchi za kiarabu na Uturuki, Yassin nchini Kuwait, waziri yassin alisema Iran ni mhusika mkubwa katika mgogoro wa Yemen na wale wanaohusika hawawezi kuwa wapatanishi.

Wakati huo huo, Saudi Arabia imeimarisha usalama kwenye maeneo yote ya maduka ya biashara na vituo vya mafuta baada ya kupokea taarifa juu ya uwezekano wa kufanyika shambulizi. Msemaji wa wizara ya ndani Meja Jenerali Mansour al-Turki amesema hatua zimechukuliwa kukabiliana na jaribio lolote la mashambulizi la wapiganaji . Mbali na kuongoza mashambulizi dhidi ya wanagmabo wa Houthi nchini Yemen, saudi arabia pia ni mshirika katika mashambulizi ya anga yanayoongozwa na Marekani dhidi ya wapiganaji wa kundi la Dola la Kiislamu nchini Iraq.

Mnamo mwezi uliopita, balozi ndogo za Marekani katika falme hiyo zilisitisha huduma zao kwa wiki moja kwasababu ya kitisho cha usalama, na polisi wawili wa Saudi Arabia walipigwa risasi na kuuawa mwanzoni mwa mwezi huu, mjini Riyadh.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman, dpa,afp,rtr

Mhariri:Yusuf Saumu