1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yemen hali ni tete

Halima Nyanza26 Mei 2011

Raia kadhaa wameuawa kufuatia mapigano ya usiku wa kuamkia leo (26 Mei 2011) nchini Yemen, wakati mapambano ya kumuondoa madarakani Rais Ali Abdualah Saleh yakitishia kuzuka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.

https://p.dw.com/p/11OO6
Rais Ali Abdullah SalehPicha: dapd

Wizara ya ulinzi nchini Yemen imesema watu 28 wameuawa, katika mlipuko uliotokea kwenye ghala la silaha, katika mji mkuu wa nchi hiyo Sanaa.

Ghala hilo la silaha lilikuwa likimilikiwa na kundi moja la kikabila linaloongozwa na familia ya Sadiq al-Ahmar, ambapo waendesha mashtaka nchini humo wameagiza kukamatwa kwa kiongozi wa kundi hilo.

Mapigano yaliyosababisha umwagaji damu yameikumba nchi hiyo tangu siku ya Jumatatu, kati ya majeshi ya nchi hiyo na wapiganaji wanaomtii Sheikh Sadiq al-Ahmar, ambaye ameunga mkono upinzani dhidi ya rais wa nchi hiyo Ali Abdullah Saleh.

Jemen Sanaa Anti Regierungsproteste
Waandamanaji nchini YemenPicha: picture alliance/dpa

Aidha afisa wa serikali nchini humo amearifu pia kwamba makao makuu ya kituo cha televisheni cha upinzani yameteketezwa. Hata hivyo hakutoa taarifa zozote zaidi. Lakini kila upande umekuwa ukilaumu mwingine kuhusiana na ghasia hizo, ambapo upinzani umesisitizia kwamba zinaweza kuitumbukiza nchi hiyo katika mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.

Mamia ya wakaazi wa mji wa Sanaa, wamekuwa wakiukimbia mji huo, kwa matumaini ya kuepukana na machafuko hayo ambayo tayari yameshaua zaidi ya watu 40, tangu siku ya Jumatatu. Machafuko hayo pia yanatishia kuenea katika maeneo mengine ya mji huo mkuu wa Sanaa.

Mapigano hayo ya hivi karibuni yametokea zaidi katika sehemu ya kaskazini mwa mji huo mkuu wa Yemen ambako wapiganaji wanaomtii kiongozi wa kikabila mwenye nguvu, Sadiq al-Ahmar wamekuwa wakijaribu kudhibiti majengo ya serikali, ikiwemo wizara ya mambo ya ndani.

Mapigano makali ya hivi karibuni yametokea siku moja baada ya Rais Saleh, ambaye ameitawala nchi hiyo kwa miaka 33, kujiondoa tena kwa mara ya tatu katika makubaliano yanayosimamiwa na nchi jirani za ghuba ya yeye kujiuzulu na kutoa njia ya kuunda serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Marekani na Saudi Arabia, ambazo kwa pamoja zimekuwa zikikabiliana na mashambulio yanayofanywa na tawi la al Qaeda lenye makaazi yake nchini Yemen, zimekuwa zikijaribu kutuliza mzozo huo na kuzuia kuenea kwa uasi ambao unaweza kutoa nafasi zaidi kwa mtandao huo wa kigaidi kuendesha shughuli zake nchini humo.

Wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani imeonya kuwa kitisho cha usalama kiko juu kutokana na ghasia zinazoendelea nchini humo na ugaidi pia.

Kutokana na kitisho kilichopo nchini humo, tayari Marekani imewaagiza maafisa wake wa kibalozi wasio wa lazima na familia za wafanyakazi wa ubalozi kuondoka nchini humo.

Mwandishi: Halima Nyanza(Reuters, IPS)

Mhariri:Josephat Charo