1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yemen yasambaratika zaidi miaka 30 baada ya Muungano

Amina Mjahid
22 Mei 2020

Miaka 30 baada ya muungano, Yemen ipo katika hatari kubwa ya kusambaratika kufuatia migogoro ya mara kwa mara, migongano ya kimaeneo na mataifa ya kigeni kuingilia mgogoro wa taifa hilo la Mashariki ya Kati.

https://p.dw.com/p/3ccLN
Jemen Sanaa Menschen hinter Flagge
Picha: picture-alliance/AP Photo/H. Mohammed

Tarehe kama ya leo Mei 22 mwaka 1990 viongozi wa iliyokuwa Yemen ya Kaskazini na Kusini zilitangaza kutoka mji mkuu wa Sanaa, kuanzishwa au kuundwa kwa Jamhuri mpya ya Yemen, hatua ambayo ilionekana kuwa ndoto iliyotimia kwa kizazi kizima cha Yemen.

Lakini miaka 30 baadae ndoto hiyo imepotea na taifa hilo limegeuka kuwa uwanja wa mapambano wa makundi yanayohasimiana.

Kunzia mwaka 2014 taifa hilo limetumbukia katika mapigano ya wenyewe kwa wenyewe kati ya serikali inayoungwa mkono na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia na waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran, ambao kwa sasa wanalidhibiti eneo kubwa la kaskazini mwa nchi hiyo pamoja na mji mkuu Sanaa.

Serikali kwa upande wake bado inashikilia eneo la kati la Marib na mikoa mengine ya Mashariki huku eneo la Kusini likiwa mikononi mwa Baraza la watu wanaotaka kujitenga STC ambalo limekuwa wazi kuwa lina nia ya kujitwalia eneo lake na kulitangaza kama taifa huru.

Mpaka sasa maelfu ya watu wameuwawa kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Yemen hatua iliyoufanya Umoja wa Mataifa kutangaza kuwa taifa hilo huenda likashuhudia mgogoro mbaya zaidi wa kiutu ambao haujawahi kuonekana duniani.

Je kuna chochote cha kusherehekea katika maadhimisho ya muungano huu?

Jemen Darwan Flüchtlingslager
Picha: picture-alliance/AA/M. Hamoud

Kulingana na mchambuzi wa siasa za kimataifa Ahmed Rajab huu ni muungano uliowaunganisha watu wa Yemen wa Kaskazini na Kusini kuwa wamoja japokuwa serikali zao hazijawahi kuwa moja, lakini hisia za watu wa kusini za kutaka kujitenga ndio changamoto kubwa inayotishia muungano huo.

Ahmed Rajab ameongeza kuwa vita vya Yemen ni vita vilivyokusanya mambo mengi na ni vigumu kulaumu sehemu mbili za kusini na kaskazini kuwa ndizo zilizoanzisha mapigano yanayoshuhudiwa sasa. Vita baina ya serikali ya Yemen ya Kaskazini na mahasimu wake wakubwa ambao ni wapiganaji wa Houthi wa sehemu za kaskazini pia, viliathiri zaidi mahusiano kati ya pande hizo mbili.

Mbali na hisia za kizalendo za wananchi wa Yemen ya kusini wanaotaka kujitenga kuna pia makundi ya watu wanaoipinga serikali ambalo ni jambo ambalo linaathiri pia uimara wa muungano huo.

kauli za watu wanaotaka kujitenga huenda zikaisambaratisha zaidi serikali iliyo mashakani

Jemen Aden Soldaten des Southern Transitional Council (STC)
Picha: picture-alliance/Photoshot/M. Abdo

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema kauli za watu wanaotaka kujitenga zinazoshinikiza lengo lao la kuhakikisha wanajitawala wenyewe,  zinatatiza na kuiweka katika matatizo zaidi serikali ambayo imeporomoka, kwa sababu inakuwa inakabiliwa na wapiganaji wa kaskazini wa Houthi, watu wanaotaka kujitenga wa kusini mwa Yemen na vile vile mashambulizi ya kigaidi ambayo yapo Yemen Kusini.

kwa sasa kumekuwa na hali ya kutokuwa na uimara baina ya Yemen mbili. Eneo la kusini limezorota kimaendeleo hadi kufikia hatua watu wake wakaona kwamba ni bora ijitenge ili wanusuru utu wao na eneo lao.

Huku hayo yakiarifiwa taifa hilo la Mashariki ya Kati linakabiliwa na janga la virusi vya corona lililosababisha vifo vya watu 20.

Kuna hofu kwamba virusi hivyo vikiendelea kuenea nchini humo huenda mfumo wa afya ambao tayari ni dhaifu ukasambaratika zaidi. Wachambuzi wanaendelea kusema kuwa bado kuna kazi ni kubwa inayopaswa kufanywa kuelekea amani na utulivu wa taifa hilo.

Chanzo: Amina Abubakar