1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yokohama: Afrika yalalama kwamba hakuna usawa wa kibiashara duniani

Mwakideu, Alex28 Mei 2008

Vingozi wa Afrika wameshutumu nchi tajiri kwa kushindwa kuweka usawa wa kibiashara duniani licha ya kuahidi kuongeza misaada.

https://p.dw.com/p/E7Y4
Mmoja wa viongozi wa Afrika Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania ambaye pia ni mweyekiti wa Umoja wa Afrika anaehudhuria kongamano la YokohamaPicha: AP Photo

Kwa upande mwengine Japan imeahidi kutumia uwezo wake wa kiteknolojia kuongeza mazao ya mchele barani Afrika katika kipindi cha muongo mmoja ili tatizo la kuongezeka kwa bei ya chakula lipungue Afrika. Yote hayo yamesemwa katika kongamano la siku tatu linalokutanisha viongozi wa nchi 40 za Afrika mjini Yokohama Japan.


Mada katika kongamano hilo ni maendeleo ya kiuchumi, utulivu na mabadiliko ya hali ya hewa.


Lakini siku ya kwanza ya kongamano hilo imeshuhudia nchi za Afrika zikilalama kuhusu bei za usafirishaji wa bidhaa kutoka Afrika hadi nchi za ng'mbo. Viongozi wa Afrika wamezitaka nchi zilizoendelea kupunguza kiwango cha pesa kinachohitajika kwa usafirishaji wa chakula, kahawa na bidhaa zinginezo.


Baadhi ya viongozi wa Afrika wamesema nchi zao hazina tatizo la chakula bali zinatatizika na ukosefu wa haki katika biashara ya kitamataifa.


Rais wa Uganda Yoweri Museveni amesema wakati dunia inakabiliwa na tatizo la chakula na nishati, Uganda inakabiliwa na tatizo lengine tofauti kwani nchi hiyo ina chakula kingi lakini haina soko la kimataifa la kukiuza kwasababu ya sera mbaya za biashara zilizoko ulaya, Marekani, na hata Japan.


Akieleza zaidi matatizo yanayoikabili nchi hiyo Museveni alitoa mfano wa kilo moja ya kahawa ambayo bado haijasafishwa akisema inauzwa kwa dola moja nchini Uganda lakini inaposafishwa na kupelekwa nchini Uingereza inapanda bei na kuwa dola 14. Jambo ambalo lilimfanya azikejeli nchi tajiri akisema anashangaa ni nani anaemsaidia mwenzake.


Kwa upande wake Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete ambaye pia ni mwenyekiti wa Umoja wa Afrika amesena maendeleo ya kiuchumi hayawezi kutokea iwapo serikali hazitaweka sera nzuri za kibiashara "Maswala mawili muhimu ambayo tumejifunza, kwanza Kwanza kuna umuhimu wa kuwa na sera nzuri, mipango, na mikakati, kwa ajili ya ukuaji wa uchumi. Njia tulizotumia, matokeo yake yalikuwa ni kukwama badala ya kuendelea" Kikwete alisema.


Wanaharakati wa kupigania biashara ya haki wanasema wakati nchi maskini zimelazimishwa kufungua wazi masoko yake, nchi tajiri zimeweka mikakati isiokuwa na haki huku kampuni za kimataifa zikishindwa kuwapatia wakulima haki yao.


Akiongea kuhusu ukuaji wa uchumi waziri mkuu wa Ethiopia Meles Zenawi aligusia swala la miundo mbinu akisema kwamba ni muhimu katika harakati za kuukuza uchumi wa Afrika "uwekezaji wa miundo mbinu Afrika umepuuzwa, katika kipindi cha miongo miwili iliyopita, na punde tuu uchumi wetu unapoanza kukua basi miundo mbinu inaurejesha nyumba" Zenawi alisema.


Rais wa Gabon Omar Bongo Ondimba ameitaka Japan ianzishe uwekezaji wa moja kwa moja barani Afrika na ifungue soko ili bidhaa kutoka Afrika ziweze kuuzwa nchini humo. 


Kongamano la Yokohama mji ulioko karibu na Tokyo, linaonekana kama jaribio la Japan la kuingia zaidi katika soko la Afrika ambalo China na India pia zinalinyemelea.


Kando na kuahidi kuongeza mazao ya mchele barani Afrika, Japan imesema itatumia bilioni 2.5 kuzisaidia kampuni zake ziendeleze biashara barani Afrika jambo ambalo litapelekea kuanzishwa kwa uwekezaji wa kibinafsi uliotajwa kuwa jambo muhimu na baadhi ya viongozi wa Afrika.