1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zanzibar yaendelea kuwatunza wazee kwa makaazi, posho

Mohammed Khelef
2 Oktoba 2018

Tangu Mapinduzi ya 1964, visiwa vya Zanzibar vimekuwa na mfumo maalum wa kuwatunza wazee wasiojiweza kupitia mradi wa kuwaweka kwenye makaazi ya pamoja na hivi karibuni kuanzisha utaratibu wa kuwalipa posho.

https://p.dw.com/p/35qyE
Sansibar Algenbäuerin Algensammlerin
Picha: DW/St. Duckstein

Pamoja na kuwa na nyumba maalum za kuwatunza wazee kupitia tamko la Rais wa Kwanza wa Zanzibar Abeid Karume, Serikali ya Zanzibar iliamuwa kuanza pia kuwalipa wazee wote wenye umri kuanzia miaka 70 na kuendelea kila mwisho wa mwezi.

Malipo haya yaliyoanza kutolewa mwaka 2016 ni shilingi 20,000 za Kitanzania, sawa na dola 9 za Kimarekani, kiwango kidogo sana cha pesa kulinganisha na hali ya maisha, lakini ni hatua iliyopongezwa ndani na nje ya nchi, wakiwemo washirika wa maendeleo.

Hata hivyo, kama kwengineko kote, kwa visiwa hivi vya Bahari ya Hindi nako pia wazee wanakabiliwa na changamoto kadhaa. Mojawapo ikiwa ni huduma za afya, hata kwenye nyumba maalum zilizowekwa kwa ajili yao na serikali.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazee Zanzibar, Bi Ghanima Mussa, anasema wamekuwa wakiomba kupewa vitambulisho maalum watakavyoweza kutumia na kupewa kipaumbele katika hospitali zote za serikali, lakini hadi sasa bado.

Changamoto nyengine kwa wazee, hasa wale waliopo kwenye nyumba maalumu, ni kukosa damu za kuwekewa pindi wanapolazwa hospitali na kuhitajika huduma hiyo.

Mwaka huu, Benki ya Damu Zanzibar iliandaa siku maalumu ya uchangiaji damu kwa ajili ya wazee, kwa mujibu wa meneja wa damu salama, Hamad Magarawa.

Kudharauliwa kwa wazee

Licha ya Zanzibar kuwa jamii ya kidini na viongozi wa dini kutumia mahubiri yao kuwataka vijana kuwatunza wazee, bado suala la kuwapuuza wazee linaonekana lipo kwa baadhi ya familia kushindwa kuwatunza wazazi wao, kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Ustawi wa Jamii, Hamida Maabad.

Zanzibar inakadiria kuwa na wazee zaidi ya 30,000 wenye umri kuanzia miaka 70, Umoja wa Mataifa unakadiria wazee duniani kuwa zaidi ya milioni 600 na idadi hiyo inakadiriwa kuongezeka kwa 17% kufikia mwaka 2050. 

Siku ya wazee duniani ilipitishwa rasmi tarehe 14 Disemba 1990 na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, kuwa kila ifikapo Oktoba 1 ya kila mwaka iwe siku maalum ya kuwakumbuka wazee. Kwa mara ya kwanza siku hii iliadhimishwa tarehe 1 Oktoba 1991.

Kaulimbiu ya mwaka huu ni "Kusherehekea wazee wanaharakati wa haki za binadamu" ili kutathmini juhudi za wazee wote katika kushajiisha kulindwa kwa haki za binanadamu duniani.

Mwandishi: Salma Said, DW Zanzibar
Mhariri: Mohammed Khelef