1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zanzibar yakabiliwa na ukiukwaji wa haki za binadamu

15 Juni 2017

Zanzibar imetajwa kukabiliwa na ukiukaji mkubwa wa haki za binaadamu, katika ripoti iliyotolewa na shirika la haki za binaadamu, ikiungana na nchi nyingine duniani kukabiliana na madhila kama hayo.

https://p.dw.com/p/2elwh
Tansania Sansibar Pemab Polizisten in Mannschaftswagen
Picha: picture-alliance/dpa

Wakati wanaharakati wa haki za binaadamu wakiwemo wa Shirika la kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch wakiendelea kulalamika kuwepo kwa ukiukwaji wa haki za binadam katika nchi mbali mbali duniani, Zanzibar pia imetajwa leo katika ripoti kuwa inakabiliwa na hali kama hiyo. 

Katika ripoti inayoangazia haki za binaadamu Zanzibar, watayarishaji wa ripoti hiyo kutoka "kituo cha huduma za sheria" wasema bado utekelezaji wa haki ni tatizo ambapo udhalilishaji, mauaji, watu kupigwa, na matumizi mabaya ya madaraka bado vinaongoza katika ukiukwaji wa haki.

 

Akizindua ripoti hiyo mjini Zanzibar kwa watu kutoka sekta ya umma na binafsi, Mwanasheria maarufu Jaji Mshibe Ali Bakar alisema kila kukicha haki za binadamu zinaendelea kukiukwa katika ngazi zote na kuathiri zaidi watu maskini. 


Alisema mara nyingi wakati wa uchaguzi kinachoangaliwa ni ule uchaguzi wenyewe lakini ili ujue uchaguzi mzuri ni kuangalia utaratibu mzima wa uchaguzi kuanzia uandikishaji, kampeni za uchaguzi na kutangazwa matokeo yenyewe

.

Ripoti hiyo pia imeelezea haki za mtoto zinavyokanyagwa na masuala ya ubakaji yalivyokithiri katika visiwa vya Unguja na Pemba huku mahakama zikilaumiwa kwa kuzifuta kesi nyingi kwa kukosekana ushahidi na katika hilo.

 

Katika ripoti hiyo imetajwa kuwa idadi ya watu waliouliwa imeongezeko kutoka wanne Mwaka 2015 hadi mauaji 34 Mwaka jana, Pamoja na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi juu ya haki zao kubinywa.

 

Akitoa maoni yake mbele ya hadhara hiyo Rais wa chama cha wanasheria Zanzibar Omar Said Shaaban aliipongeza ripoti hiyo lakini akashauri wadau wapewe muda wa siku nzima wa kuipokea na siku ya pili kuijadili.


Katika ripoti hiyo pia limetajwa suala la uhuru wa mahakama katika kufanya kazi zake na kutaja haki ya washitakiwa kupewa dhamana katika kesi za jinai.

 

Mwandishi: Salma Said.

Mhariri: Josephat Charo