1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waingereza wasubiri kuamua

23 Mei 2016

Mazungumzo ya kansela Angela Merkel na rais wa Uturuki Erdogan uchaguzi wa rais nchini Austria na kura ya maoni itakayoamua kama Uingereza ibakie au ijitoe katika Umoja wa Ulaya ni miongoni mwa mada magazetini.

https://p.dw.com/p/1Issd
Rais Recep Erdogan alipokutana na kansela Angela Merkel mwaka 2013 mjini IstanbulPicha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Tuanzie na ziara ya kansela Angela Merkel nchini Uturuki. Kishindo cha wakimbizi na pia kitisho cha Uturuki kugeuza njia baada ya bunge kuunga mkono wabunge zaidi ya 100 wapokonywe kinga ni miongoni mwa visa vinavyowakosesha usingizi viongozi wa nchi za Umoja wa ulaya. Gazeti la "Hannoversche Allgemeine" linasema hii si mara ya kwanza kwa kansela Merkel kufika ziarani Uturuki."Hii ni mara ya tano katika kipindi cha miezi saba Kansela Merkel anakwenda Uturuki. Diplomasia hii ya ziara ina mipaka yake kwasababu majadiliano pamoja na kiongozi wa nchi mfano wa Erdogan daima hugeuka kuwa adha kwa kansela Merkel. Miezi michache iliyopita alilazimika kuitegemea Uturuki ili kupunguza idadi ya wakimbizi wanaoingia Ujerumani.

Shinikizo kubwa upande huo lilitokea katika jimbo la kusini la Bavaria. Na safari hii pia waziri mkuu wa jimbo hilo Horst Seehofer anamshinikiza kansela anapokwenda ziarani mjini Istanbul: Merkel anabidi aitanabahishe Uturuki irejee katika njia ya kidemokrasi. Na kwakua shinikizo la kwanza halilingani na la pili,tayari kuna wanaoashiria,ni nani mbali na Erdogan atakaefurahia kuvunjika makubaliano pamoja na Uturuki kuhusu wakimbizi.

Siku ya siku ya wadia waingereza wataamua

Kura ya maoni itakayowafungulia njia waingereza kutamka kama wanataka kuendelea kuwa wanachama wa umoja wa Ulaya au la-mashuhuri kwa jina la mkato-Brexit inakaribia. Na kila siku zinavyokaribia ndipo nao wahariri wanavyozidi kuichambua mada hiyo. Gazeti la Mittelbayerische la mjini Regensburg linaandika:"Obelix angesema: Ah,hawa waingereza wanazo lakini? Wiki karibu nne ndizo zilizosalia hadi kura ya maoni itakapoitishwa na kuamua kuhusu hatima ya Uingereza katika Umoja wa Ulaya na mpaka sasa bado zaidi ya asili mia 40 ya wakaazi wa visiwa hivyo wanahisi itakuwa vizuri wakitoka. Ndo kusema hawakusikia? Kujitenga na soko la pamoja la wanunuzi 500 milioni? Au hawataki kujua kitakachowafika?"

Waustria wasubiri kumjua rais wao

Mada yetu ya mwisho magazetini inahusu kitandawili cha uchaguzi wa rais nchini Austria. Baada ya kuhesabiwa kura zilizopigwa ndani nchini humo, mshindi bado hajulikani kati ya wagombea wawili wa kiti cha rais Norbert Hofer wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia na Van der Bellen wa walinzi wa mazingira. Wanabidi wasubiri kura za waustria wa ughaibuni kuweza kujua Austria inaelekea wapi. Gazeti la "Der neue Tag la mjini Weiden linaandika:"Kimoja lakini ni bayana tangu uchaguzi huo ulipomalizika: Jamhuri hiyo ya milima ya Alpes imegawika zaidi kuliko nchi yoyote nyengine ya Umoja wa Ulaya. Kwa upande mmoja wafuasi wa siasa kali ya mrengo wa kulia na ambao leo hii hawavai tena viatu vya wapanda farasi na makoti meusi yaliyotuna mgongoni, bali wanavaa suti na wepesi wa kupendekeza nini cha kufanya kukabiliana na matatizo. Na upande wa pili wanakutikana wale wanaohisi kuwa demokrasia ndio mfumo bora kwa watu wenye maoni tofauti. Kama mfarakano huo unasawazika?

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman