1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ziara ya Angela Merkel mjini Sochi.

Sekione Kitojo14 Agosti 2009

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amekutana na rais Dmitry Medvedev leo na viongozi hao wametoa wito wa kujenga uhusiano wa ndani zaidi wa kiuchumi kwa ajili ya nchi zao.

https://p.dw.com/p/JBRO
Rais wa Urusi Dmitri Medvedev akizungumza na waziri wake mkuu Vladimir Putin.Picha: AP

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amekutana na rais Dmitri Medvedev leo na viongozi wote wawili wametoa wito wa kuwa na uhusiano wa ndani zaidi wa kiuchumi huku kukiendelea kuwa na mazungumzo ya makubaliano kadha makubwa ya kiviwanda kati ya nchi hizo mbili.

Akizungumza na waandishi habari wakati akimlaki kansela Merkel katika makaazi yake katika bahari ya Black Sea, Medvedev alimpongeza Merkel kutokana na taarifa kuwa Ujerumani imeondoka katika mporomoko wa uchumi na kusema Urusi inafanya juhudi kwa nguvu zake zote kufikia lengo kama hilo.

Tunapaswa kufikiria vipi , kwa kuimarisha mikakati ya ushirikiano wetu wa kiuchumi , tunaweza kusaidia uchumi wa nchi zetu na watu kuepuka athari za mzozo huu duniani na kujikuta tukiwa imara baadaye, amesema rais Medvedev.

Merkel amejibu kwa kusema kuwa amefurahishwa sana na habari za uchumi wa Ujerumani zilizotolewa siku ya Ijumaa na kuthibitisha kuwa mkutano wake na Medvedev , ukiwa mkutano wa pili katika muda wa karibu mwezi mmoja na wa tatu katika mwaka huu, utatuwama katika masuala ya kiuchumi.

Naamini kuwa tunahitaji kutumia kila nafasi ambazo mzozo huu wa kiuchumi duniani unazitoa kuendeleza uhusiano wa kiuchumi kati ya Urusi na Ujerumani, ameongeza kansela wa Ujerumani.

Merkel anatarajiwa kubakia kileleni mwa nchi hiyo yenye uchumi imara katika bara la Ulaya kufuatia uchaguzi utakaofanyika septemba 27 na Medvedev amesema yeye pamoja na kansela wa Ujerumani pia wamejadili masuala ya kimataifa.

Kansela Merkel amesema kuwa anapendelea zaidi jaribio linaloungwa mkono na Urusi la kampuni ya Magna kutaka kuinunua kampuni ya Opel.

Akizungumza baada ya mazungumzo na rais Medvedev , Merkel amesema majadiliano kuhusiana na hali ya baadaye ya Opel hivi sasa yamefikia kiwango muhimu. Anamatumaini ya kufikiwa uamuzi haraka iwezekanavyo. Merkel pia ametoa wito wa kutolewa shutuma kali dhidi ya matukio ya hivi karibuni ya mauaji katika jimbo la Urusi la Chechnya , ikiwa ni pamoja na mauaji ya mkuu wa shirika la kutoa misaada kwa watoto Zerema Sadulayeva.

Wakati huo huo Urusi haiwezi kurejesha uhusiano wa kawaida na Ukraine chini ya utawala wa sasa wa nchi hiyo, amesema rais Dmitry Medvedev. Amesema kuwa haoni uwezekano wa kurejesha uhusiano wa kawaida chini ya viongozi wa sasa nchini Ukraine, Medvedev amesema katika mkutano wa pamoja na waandishi habari.