1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ziara ya Bush nchini Israel

Hamidou, Oumilkher15 Mei 2008

Rais Bush anaashiria maadhimisho ya miaka 120 ya kuundwa dola la Israel

https://p.dw.com/p/E0GM
Rais Bush na waziri mkuu OlmertPicha: AP


Mnamo siku ya pili ya ziara yake nchini Israel,inakosherehekewa miaka 60 tangu taifa hilo la kiyahudi lilipoundwa,rais George W. Bush ameizuru hii leo ngome ya Massada inayotukuzwa kama kitambulisho cha mapambano na  tambiko.



Rais George W. Bush akifuatana na waziri mkuu Ehud Olmert walisafirishwa kwa treni  inayopita juu kwa juu milimani hadi katika bonde la Massada ambako,kwa mujibu wa maandishi ya karne ya kwanza kabla ya enzi zetu,wazeloti 960 wa kiyahudi,tangu wanaume,mpaka wanawake na watoto waliamua kujiuwa ili waepukane na kujisalimisha kwa vikosi vya warumi waliokua wakiwazingira.


"Moyo na ushujaa wa wale waliopigana Massada wanao pia waisrael wa leo" amesema hayo msemaji wa rais Bush,Dana Perino.


Ngome hiyo ya kale imejengwa jangwani,kusini mwa mji wa Jerusalem.


Rais Bush amelitembelea eneo hilo kabla ya wapalastina kuadhimisha "Nakba"-pale jamaa zao laki saba na 70 elfu walipoyapa kisogo maskani yao na kukimbilia uhamishoni siku chache baada ya kuundwa taifa la Israel.


Rais George W. Bush anatazamiwa baadae hii leo kuhutubia mbele ya bunge la Israel Knesset.


Nakala ya hotuba yake iliyowafikia waandishi habari inazungumzia mara moja tuu juu ya wapalastina, na hakuna mstari wowote unaodhukuru matumaini ya rais Bush ya kufikiwa makubaliano ya amani kati ya Israel na Palastina kabla ya mhula wake huu wa pili kumalizika mwezi january mwakani.


Badala yake anagusia jinsi eneo la mashariki ya kati litakavyokua miaka 60 kutoka sasa,akiashiria maadhimisho ya miaka 120 ya kuundwa dola la Israel,analolisifu kama mojawapo ya madola makubwa ya kidemokrasia katika sayari yetu na kwamba wapalastina watajipatia nchi yao wanayoistahiki na ambayo wamekua wakiiotea kwa muda mrefu .


Hata hivyo rais Bush anasema:


""Nitazungumzia siku ambayo nnamini kila mtoto wa mashariki ya kati ataweza kuishi kwa amani na kua huru."


Atazungumzia pia kuhusu Iran-adui mkubwa wa Israel katika eneo hilo.


"Kuiachia nchi inayounga mkono ugaidi,imiliki silaha za kinuklea litakua kosa kubwa la uhaini  ambalo hakuna kizazi chochote kinachoweza kulisamahe."Anatarajiwa kusema rais Bush wakati wa hotuba yake katika bunge la Israel hii leo.


Katika wakati ambapo rais George W. Bush anaendelea na ziara yake nchini Israel, wanajeshi wa Israel waliowekwa Erez wako katika hali ya tahadhari baada ya Hamas kuwatolea mwito wakaazi wa Gaza walivamie eneo hilo.


Kombora lililovurumishwa jana toka Gaza lilipiga katika kituo cha kibiashara cha Ashkelon nchini Israel na kuwajeruhi watu kadhaa.Shambulio hilo lilijiri wakati rais George W. Bush alipokua akikutana na waziri mkuu Ehud Olmert mjini Jerusalem.