1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ziara ya kansela Merkel barani Afrika

Oummilkheir5 Oktoba 2007

Kansela Angela Merkel azungumza na rais Thabo Mbeki kuhusu hali ya Zimbabwe

https://p.dw.com/p/C785
Picha: AP

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amekua na mazungumzo hhi leo pamoja na rais Thabo Mbeki wa Afrika kusini, mjini Pretoria.Mbali na uhusiano wa pande mbili,viongozi hao wawili wamezungumzia pia hali nchini Zimbabwe.

Katika kituo cha pili cha ziara yake barani Afrika,kansela Angela Merkel amekua na mazungumzo hii leo pamoja na rais Thabo Mbeki wa Afrika kusini.Mazungumzo yao yalituwama zaidi katika suala la Zimbabwe na juhudi za Afrika kusini katika kusaka ufumbuzi wa mizozo ya bara la Afrika.Kansela Angela Merkel amemsihi mwenyeji wake,azidi kumshinikiza rais Robert Mugabe ahakikishe haki za binaadam zinaheshimiwa nchini humo.

Kansela Angela Merkel anasema:

“Mzozo wa Zimbabwe ni mfano mmoja wapo wa kuvunjwa haki za binaadam.Tumeingiwa na hofu kutokana na hali namna ilivyo,jinsi watu wanavyosumbuliwa,wanavyotishwa,jinsi wapinzani wanvyotiwa kishindo,mitaa ya wasiojimudu inavyovunjwa na jinsi haki za binaadam zinavyoendelea kuvunjwa.Hatustahiki kupakata mikono mbele ya hali kama hiyo.“

Rais Thabo Mbeki anaejaribu kuzileta pamoja serikali ya Zimbabwe na upande wa upinzani,amesema tunanukuu:“maendeleo yameanza kupatikana.“Mwisho wa kumnukuu.Hata hivyo rais Mbeki amemhakikishia mgeni wake Afrika kusini itafanya kila liwezekanalo ufumbuzi wa amani upatikane nchini Zimbabwe.

Mjadala unaotokana na hoja kama rais Robert Mugabe ashiriki au la katika mkutano wa kilele wa Umoja wa ulaya na Afrika umeutia nukhsi uhusiano kati ya Ulaya na Afrika.

Serikali kuu ya Ujerumani imesema hivi karibuni kansela Angela Merkel atahudhuria mkutano huo wa kilele uliopangwa kuitishwa december ijayo nchini Ureno,kinyume na waziri mkuu wa uengereza Gordon Brown aliyeamua kuususia mkutano huo wa kilele ikiwa rais Robert Mugabe atahudhuria.

Baada ya mazungumzo yao,kansela Angela Merkel alimhakikishia rais Mbeki uungaji mkono wa Ujerumani kwa maandalizi ya michuano ya fainali za kombe la dunia la kabumbu mwaka 2010 nchini Afrika kusini.

Leo jioni kansela Angela Merkel akifuatana na ujumbe wake akiwemo pia meneja wa timu ya taifa ya kabumbu nchini Ujerumani Oliver Bierhoff ,anautembelea uwanja mkuu wa michezo unaojengwa makusudi kwaajili ya fainali hizo za kombe la dunia.

Kesho kansela Angela Merkel ataonana na rais mstaafu wa Afrika kusini Nelson Mandela kabla ya kwenda Cape Town kuzuru miradi ya kupambana na ukimwi na ulinzi wa mazingira.

Kansela Angela Merkel atakamilisha ziara yake nchini Liberia ambako jumapili ijayo amepangiwa kuzungumza na rais Ellen Johnson Sirleaf.