1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ziara ya Kansela na Baraza lake la Mawaziri Israel

26 Februari 2014

Kumalizika kikao cha mazungumzo kati ya baraza la mawaziri la Ujerumani na lile la Israel ,hatua za kufunga mkaja za serikali ya Marekani na bajeti ya Ujerumani ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa zaidi magazetini

https://p.dw.com/p/1BFU4
Kansela Angela M erkel akiamkiana na rais wa Israel Shimon PeresPicha: Reuters

Tunaanzia Tel Aviv yalikomalizika hapo jana mazungumzo kati ya serikali za Israel na Ujerumani.Gazeti linalosomwa na wengi "Bild" linahisi ziara hiyo imefana.Bild linaendelea kuandika:"Kwa Angela Merkel na baraza lake la mawaziri ziara hii ilikuwa ya maana.Sio tu kwasababu kansela amekuwa mjerumani wa kwanza kutunukiwa nishani yingi zaidi za nchi hiyo.Hiyo ni hishma kubwa bila ya shaka,lakini cha kusisimua zaidi ni jinsi alivyopokelewa nchini Israel.Na hayo yanatokea katika wakati ambapo kansela hajawahi kuwaficha waisrael.Kinyume kabisa:Alitamka bayana kuhusu ufumbuzi wa madola mawili na kuzungumzia kinaga ubaga kuhusu hofu za wajerumani kuelekea ujenzi wa makaazi mepya ya wayahudi katika ardhi za wapalastina.Na Licha ya yote hayo hakuacha hata mara moja kushadidia mshikamano wa dhati wa Ujerumani na Israel.Kuna tofauti mtu anaweza kusema kati ya lawama zilizotolewa na kansela Angela Merkel na zile alizotowa hivi karibuni spika wa bunge la ulaya Martin Schulz katika bunge la Israel Knesset.Angela Merkel ameifanya Ujerumani ithaminiwe zaidi nchini Israel."

Gazeti la "Lausitzer Rundschau" linazungumzia jinsi Ujerumani inavyoweza kuchangia katika juhudi za kuleta amani Mashariki ya kati.Gazeti linaendelea kuandika:"Berlin inaweza na inabidi isaidie katika utaratibu wa amani ya Mashariki ya kati.Inaweza kutathmini na kusimamia juhudi za kufikia amani.Ili kuweza kutekeleza jukumu hilo serikali kuu ya Ujerumani inabidi itumie werevu na mbinu za kidiplomasia.Ujumbe unaotokana na ziara iliyomalizika jana mjini Jerusalem unamaanisha "Sisi ni marafiki zenu na sio wapinzani wenu hata kama tunazungumza na wapinzani wenu."

Marekani yafunga Mkaja

Hatua za serikali ya Marekani za kupunguza matumizi zimemulikwa pia na wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanaohisi hasa hatua za kupunguza matumizi katika wizara ya ulinzi zitaziathiri pia nchi za Ulaya.Gazeti la "Der Neue Tag" linaandika:"Kwakua waziri wa ulinzi Chuck Hagel anaendelea kuzidisha makali ya hatua za kufunga mkaja jeshini,hapatapita muda Ulaya pia itakabiliana na kishindo cha hatua hizo.Seuze uamuzi wa kufungwa kambi za kijeshi utabidi uidhinishwe na bunge la Marekani Congress.Wabunge watazitaka nchi za ulaya nazo pia zipitishe hatua zinazostahiki.Mjini Washington tokea hapo viongozi wamekasirishwa na washirika wao.Wabunge wanawataka washirika wao wa Ulaya wadhamini wenyewe ulinzi wao.Wanafika hadi ya kuwakosoa wanashindwa hata kutekeleza majukumu yao katika jumuia ya kujihami ya NATO."

USA U. S. Army soll deutlich kleiner werden Chuck Hagel und Martin Dempsey
Waziri wa Ulinzi wa Marekani Chuck Hagel na Mkuu wa vikosi vya Wanajeshi Martin DempseyPicha: Reuters

Bajeti ya Ujerumani yasawazika

Ripoti yetu ya mwisho magazetini inahusu matarajio mema ya kiuchumi kwa Ujerumani.Gazeti la "Badische Neueste Nachrichten" linaandika:"Mkataba wa kuunda serikali ya muungano hauzungumzii sana kuhusu hatua za kufunga mkaja,lakini kuhusu gharama mpya kwa matumaini kwamba mapato ya kodi yataendelea kumiminika.Hata hivyo Angela Merkel,Sigmar Gabriel na Horst Seehofer wangefanya la maana kama wangechemsha bongo zaidi badala ya kutegemea matunda ya zamani."

Bundestag Sitzung Diäterhöhung 21.02.2014
Wabunge wa Ujerumani wakizungumzia nyongeza za mishaharaPicha: Reuters

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri. Mohammed Abdul-Rahman