1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ziara ya Kansela wa Ujerumani katika Nchi za Baltik

P-Stützle(P.martin)25 Agosti 2008

Ziara ya Kansela wa Ujerumani Angela Merkel hii leo na kesho Jumanne nchini Sweden,Estonia na Lithuania ilipangwa kama ziara ya kawaida tu.

https://p.dw.com/p/F4Fv

Lakini kufuatia vita vya Kaukasus ziara hiyo inafanywa katika mazingira yalio tofauti:kwani serikali za nchi tatu anazozizuru zimechukua msimamo mkali kuhusu uvamizi wa Urusi nchini Georgia,huku Ujerumani na hata Ufaransa zikijitahidi kuwa na msimamo wa wastani dhidi ya Moscow.

Ni dhahiri kuwa mada kuu katika majadiliano ya Kansela Merkel wakati wa ziara yake ya siku mbili nchini Sweden,Estonia na Lithuania haitohusika na sera za kilimo za Ulaya bali mzozo wa Georgia na uhusiano wa Ulaya na Moscow.Kituo cha kwanza cha ziara yake ni Sweden,nchi ambayo waziri mkuu wake Reinfeldt amesitisha kila uhusiano wa kijeshi na Moscow tangu Jumatatu iliyopita.

Kutoka Sweden Merkel siku ya Jumanne ataelekea Estonia na Lithuania.Marais wa nchi hizo mbili baada tu ya Georgia kuvamiwa na vikosi vya Urusi,walifuatana na marais wenzao kutoka Poland na Latvia hadi mji mkuu wa Georgia Tbilisi kudhihirisha uungaji mkono wao wa Rais wa Georgia Saakaschvilli.Lakini Angela Merkel na hata serikali za Ufaransa na nchi wanachama asili wa Umoja wa Ulaya walijizuia kuilaumu Urusi waziwazi badala yake walikosoa hatua zake zilizopindukia kiasi.Hivyo kumekuwepo ishara za mtengano kama ilivyokuwa kabla ya vita vya Irak.Lakini msemaji wa serikali ya Ujerumani Thomas Steg amesema:

"Hakuna suala la mtengano.Tunaamini kuwa katika siku au majuma yajayo tutafanikiwa kuwa na msimamo mmoja katika Umoja wa Ulaya."

Yaani kama vile mawaziri wa nje wa Umoja wa Ulaya walivyoweza kuwa na msismamo mmoja na kutoa taarifa ya pamoja kiasi ya majuma mawili yaliyopita.Hata hivyo bado kuna tofauti za maoni.Kwani nchi za Balkan zilizokuwa chini ya utawala wa Soviet Union ya zamani na baadae kukimbilia kujiunga na NATO katika mwaka 2004,zinadai kuwa Georgia pia ipokewe haraka kama mwanachama.Hata Kansela Merkel alipokwenda Tbilisi juma moja lililopita alizungumzia uwezekano huo.Lakini msemaji wake amesema:

" Huo si uamuzi wa kupitishwa leo au kesho."

Kwa maoni yake uamuzi wa aina hiyo haupitishwi katika mji mkuu fulani bali huamuliwa kufuatia majadiliano ya pamoja kati ya Umoja wa Ulaya na NATO iwapo masharti kadhaa yametimizwa; na chini ya msingi huo ndio kutapitishwa uamuzi wa mwisho.Ziara ya Kansela wa Ujerumani katika miji ya Stockholm,Tallinin na Vilnius huenda ikasaidia kuwapatia msimamo mmoja dhidi ya Urusi.