1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ziara ya kidiplomasia na bakteria wa E. Coli walitokea wapi?

7 Juni 2011

Wahariri hii leo wamejishughulisha na mada kadhaa zikiwemo ziara ya Kansela Merkel nchini Marekani, uamuzi wa kuacha matumizi ya nishati ya nuklia na bakteria wa E. Coli ambao mpaka sasa chanzo chake hakijajulikana

https://p.dw.com/p/11Vhz
Bunda la magazetiPicha: Fotolia/Olena Kucherenko


Mhariri wa Gazeti la Rheinische Post analiangazia suala la nishati mbadala lililojitokeza baada ya Baraza la Mawaziri kupitisha uamuzi wa kuacha matumizi ya nishati ya nuklia ifikapo mwaka 2022. Gazeti linaeleza kuwa, raia wa kawaida wa Ujerumani wanataka walipwe fidia nyingi zaidi kadri ardhi yao inavyochukuliwa kwa minajili ya kutenga nafasi za kuweka mitambo ya kutengeneza nishati mbadala.


Fidia na Thamani

Mhariri anaeleza kuwa kwa sasa, wakulima hao wanapata kiasi ya asilimia 10 hadi 20 ya thamani ya ardhi yao kwa mpigo kama fidia. Hata hivyo malipo hayo hutolewa mara moja tu. Kwa mujibu wa

rais wa shirika la wakulima wa Ujerumani, Gerd Sonnleitner, katika siku za usoni, malipo hayo yanapaswa kuenda sambamba na thamani na bei halisi ya ardhi.

Kadhalika ni vyema malipo hayo kutolewa kila wakati yaani isiwe kwa mpigo mmoja. Gazeti linamalizia kwa kueleza kuwa katika siku zijazo, serikali ya Ujerumani ina mpango wa kuuimarisha sekta ya kutengeneza nishati mbadala kwa kutumia upepo unaovuma kutoka Ziwa la Kaskazini na Mashariki. Nishati hiyo itasafirishwa hadi eneo la Kusini mwa nchi.

NO FLASH EHEC Bakterien
Bacteria wa E. Coli: Chanzo bado hakijulikaniPicha: picture alliance/dpa

Sakata la E. Coli

Kutugeuzia mada, zamu sasa ni ya Gazeti la Saabrücker Zeitung linalowasilisha suala la bakteria wa E. Coli ambao mpaka sasa chanzo chake hakijabainika. Mhariri anafafanua kuwa Waziri wa Kilimo wa Ujerumani, Ilse Aigner, ameitetea idara inayohusika na mapambano dhidi ya athari zinazosababishwa na bakteria wa E. Coli.

Gazeti la Saabrücker linaendelea kueleza kuwa idara hiyo ililaumiwa na kukosolewa sana ila katika mahojiano na gazeti hilo, Waziri Ilse Aigner alisema kuwa hatua zote mwafaka zimechukiliwa ili kuidhibiti hali. Gazeti linaendelea kueleza kuwa huu si muda wa kuwa na malumbano. Waziri huyo anautolea wito umma wa kuendelea kutokula mboga mbichi na kachumbari kama njia ya kujikinga. Hii ni kwasababu, uchunguzi unaofanywa na taasisi za Robert- Koch na ile ya serikali bado unaendelea na chanzo haswa bado hakijabainika. Gazeti linamaliza kwa kukumbusha kuwa mawaziri wa kilimo wa Umoja wa Ulaya wanakutana hii leo nchini Luxembourg ili kulijadili suala hilo kwa kina na kuzitafuta mbinu mujarab za kuapmbana na janga hilo.

NO FLASH Obama Merkel
President Barack Obama walks with German Chancellor Angela Merkel follwing their dinner at 1789 restaurant in the Georgetown neighborhood in Washington, Monday, June, 6, 2011. (Foto:Pablo Martinez Monsivais/AP/dapd)Picha: dapd

Ziara ya kunyosheana mkono?

Hatimaye, mhariri wa Gazeti la Osnabrück anapata fursa ya kuichambua ziara ya Kansela Merkel ya Marekani. Gazeti hilo linafafanua kuwa ni vigumu kueleza iwapo Rais wa Marekani Barack Obama anajitahidi kuliko inavyotarajiwa kuwa mkarimu kwa Kansela Angela Merkel. Hii ni kwasababu Kansela Merkel aliandaliwa karamu mahsusi ambayo azma yake ni kuuimarisha uhusiano kati ya mataifa yao.

Gazeti linaeleza kuwa viongozi hao wawili wako chonjo na inaelekea wanataka kuondoa hisia zozote kuwa uhusiano kati yao una dosari. Mhariri anaeleza kuwa Marekani imeshangazwa tangu uongozi wa Ujerumani kupitisha uamuzi wa kuacha matumizi ya nishati ya nuklia baada ya mkasa ulioikumba Japan. Suala jengine ni sarafu ya euro inayotikiswa na misukosuko katika sekta ya fedha barani Ulaya kwasababu ya madeni yanayozikabili nchi zinazoitumia. Jengine la msingi linaloweka kiwingu ni suala la Libya na sera za nje za Ujerumani. Itakumbukwa kuwa Ujerumani haijataka kuhusika moja kwa moja na suala la Libya ambako operesheni ya NATO inaendelea. Inavyoelekea haiko mbali na msimamo wa Urusi na China anafafanua mhariri wa gazeti la Osnabrück. Mhariri anamaliza kwa kueleza kuwa , Rais Obama hajui aegemee wapi ukiyazingatia yote hayo.

Mwandishi: Mwadzaya, Thelma-Inlands Presse-DPA

Mhariri:Abdul-Rahman