1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ziara ya Obama Ikulu Washington

11 Novemba 2008

Wahariri wamechambua kuanzia ziara ya Obama kwa Bush hata maandamano ya wapinzani wa taka za kinuklia Gorleben.

https://p.dw.com/p/FrWr
Obama na Bush (ikulu).Picha: AP

Uchambuzi wa safu za wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo, umegusia mada mbali mbali tangu za ndani ya nchi kama vile malalamiko ya waandamanaji juu ya msafara uliopakia takataka za kinuklia kutoka jaa la La Hague, Ufaransa kwenda Gorleben,Ujerumani,hata za nje kama ziara ya jana ya Rais-mteule wa Marekani Barack Obama, Ikulu mjini Washinghton na hatua zake za kwanza anazopanga kuchukua,mkutano wa kilele mwishoni mwa wiki juu ya mzozo wa fedha ulimwenguni na ujambazi wa maharamia wa kisomali katika pwani ya pemebe ya Afrika:

"Rhein-Necker-Zeitung" na changamoto za kwanza zinazomkabili rais-mteule Barck Obama:

"Kuanzia kulifunga kabisa gereza la Guantanamo,kuregeza msimamo wa Marekani juu ya mkataba wa kuzuwia kuchafuka zaidi kwa hali ya hewa,kuregeza sheria za kuharibu mimba,kuwatoza kodi za juu zaidi kwa mapato kwa matajiri,kuyaondoa haraka majeshi ya marekani nchini Irak-hakuna mada zilizouandama utawala wa George Bush ambazo Barack Obama hana nia ya kuzifanyia mageuzi makubwa na kufanya tofauti kabisa na mtangulizi wake George Bush.Mabadiliko alioahidi yabainika ameyavalia njuga na kwamba haikua porojo tupu la kampeni ya uchaguzi."

Ama Main-Post-gazeti linalotoka Wurzburg likiutupia macho mkutano wa kilele wa dola kuu 20 za kiviwanda mwishoni mwa wiki hii kuzungumzia mzozo wa fedha laandika:

"Hiki hakitakua kikao chengine tu,kwani tayari katika mkesha wake ,tumesikia visa vingi kuhusiana na mkutano huu wa kilele.Hata ikiwa msukosuko wa uchumi wa miaka ya 1930 ulioanzia na kuporomoka kwa masoko ya hisa na wa mabanki,msukosuko hasa wa kiuchumi ulikuja pale wanunuzi wa bidhaa walipoanza kutonunua bidhaa na serikali zikaangukia mtindo wa kulinda masoko yao ili kujiokoa.Kodi za juu na vikwazo vya kibiashara vikabidi kusaidia masoko yao ya kazi.....kutoka darasa hilo viongozi hawa wajifunze wanapokutana mwishoni mwa wiki hii katika mkutano wao wa kilele ambao unaweza ukaingia katika historia."

Westfalenpost linauchambua uharamia unaopita wakati huu katika pwani ya Somalia.Linasema ni ukweli wa umwagaji damu na matumizi ya nguvu unaodhihirika pwani ya Somalia ambako maharamia wanazivamia meli tangu za abiria,za mafuta hata za abiria. Gazeti la ongeza:

"Wezi hawa wa baharini wanahujumu na kuwatekanyara binadamu.Wanahatarisha misafara ya meli inayopakia shehena na njia za usafiri wa bidhaa muhimu kwa ulimwengu mzima na hata kwa ulaya.

Kitisho hiki ni cha kweli na hakiko mbali hata ikiwa inaonekana hivyo.Kwahivyo, vita hivi dhidi ya maharamia katika Pembe ya Afrika,vinatuhusu moja kwa moja."

Likitugeuzia mada, gazeti la Nordsee-Zeitung kutoka Bremerhaven, lachambua maandamano yalioibuka upya dhidi ya msafara unaopakia takataka za kinuklia:Laandika:

"Kwa jicho la kwanza unalotupa, unaona msafara huu ni kama ule wa zamani.Garimoshi iliopakia shehana ya taka za kinuklia inatoka La Hague kwenda Gorleben na maalfu ya waandamanaji na polisi wanapambana kandoni mwa msafara huo.Kwani, wapinzani wa nishati ya kinuklia wamepania tena .Lakini mwaka huu baadhi ya mambo ni tofauti na zamani.

Jaa la kutupia takataka hizo ni mgodi wa zamani wa chumvi sawa na jaa la mwisho la kutupia takataka hizo huko Gorleben.Yule anaedai mgodi wa chumvi ni kituo barabara cha kutmwaya takataka za miale ya kinuklia huyo anaota ndoto."