1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ziara ya rais wa Ufaransa Emmanuel Macron Marekani

Oumilkheir Hamidou
23 Aprili 2018

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa anaanza ziara rasmi ya siku tatu nchini Marekani . Mada tatu kuu, makubaliano ya kimataifa kuhusu mradi wa nuklea wa Iran, vita nchini Syria na biashara zitakazogubika mazungumzo yao.

https://p.dw.com/p/2wUoF
Frankreich Nationalfeiertag in Paris | Trump & Macron
Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Euler

 

Ziara ya rais Emmanuel Macron na mkewe Brigitte itaanza usiku kwa kukutana na rais Trump na mkewe Melania kwa karamu ya chakula cha usiku huko Mount Venon, makaazi ya zamani ya rais wa kwanza wa Marekani George Washington katika mji wa kusini mwa Washington,Virginia.

Mazungumzo kati ya Macron na Trump na wajumbe wao yamepangwa kuanza kesho jumanne katika ikulu ya White House na kufuatiwa na karamu rasmi itakayoongozwa na mwenyewe rais Trump.

Kwa mujibu wa duru za ikulu ya White House, jumatano inayokuja rais Emmanuel Macron atahutubia kikao cha pamoja cha mabaraza yote mawili ya bunge la Marekani Congress kabla ya kukutana na wanafunzi wa chuo kikuu cha George Washington.

Rais Macron akizungumza na rais Trump pembezoni mwa hadhara kuu ya Umoja wa mataifa mjini New-York tarehe 18.09.2017
Rais Macron akizungumza na rais Trump pembezoni mwa hadhara kuu ya Umoja wa mataifa mjini New-York tarehe 18.09.2017Picha: picture-alliance/AP Photo/E. Vucci

Macron kumtanabahisha rais Trump aregeze kamba

Katika mahojiano yaliyotangazwa jana na kituo cha matangazo cha Fox News, rais Emmanuel Macron mwenye umri wa miaka 40 amesema "ana uhusiano wa aina maalum pamoja na Trump kwasababu wote wawili ni "wageni katika uwanja wa kisiasa". Hata hivyo hitilafu za maoni kati ya Ufaransa na Marekani ni kubwa na rais Macron anataraji uhusiano huo wa aina yake utasaidia kumtanabahisha rais Trump aregeze kamba katika mada kadhaa .

Mada kuu na tete ni mkataba wa kimataifa kuhusu mradi wa nuklea wa Iran uliotiwa saini mwaka 2015. Rais Donald Trump ametishia "kuuchana" ikiwa hautofanyiwa marekebisho na kuilazimisha serikali ya mjini Teheran kupunguza mradi wake wa kutengeneza makombora ya kasi na kupunguza ushawishi wake katika eneo la mashariki ya kati. Katika mahojiano pamoja na FOX News rais Macron ametetea kuendelezwa makubaliano yaliyofikiwa japo yana kasoro ."Kama makubaliano yaliyofikiwa pamoja na Iran yamekamilika? La. Lakini kwa mradi wa nuklea, hakuna njia bora. Siiioni. Hakuna mpango mbadala wa nuklea dhidi ya Iran. Na hilo ndilo suala tutakalolijadili. Ndio maana nnataka kusema katika suala la nuklea, bora tufuate mpango huu ulioko kwasababu ni wa maana kuliko kuwa na hali kama ile iliyoko Korea ya kaskazini."

Rais Trump alipokuwa ziarani Paris mwezi julai  mwaka 2017
Rais Trump alipokuwa ziarani Paris mwezi julai mwaka 2017Picha: picture alliance/AP/M. Schreiber

 Ushuru ziada wa bidhaa ya chuma puwa kutoka Ulaya mazungumzoni

Rais Macron amepinga pia fikra ya rais Trump ya kuondowa wanajesjhi wa Marekani kutoka Syria na anapanga kuitumia ziara yake hii rasmi kushadidia mchango wa Marekani na Ufaransa katika kupambana dhidi ya ugaidi. Rais wa Ufaransa amepania pia kuzungumzia azma ya rais Trump ya kupandisha ushuru kwa bidhaa za chuma puwa zinazoagiziwa kutoka Ulaya.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/dpa/Reuters

Mhariri:Yusuf Saumu