1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ziara ya Sarkozy Afrika kaskazini

Mohammed Abdul-Rahman9 Julai 2007

Uhasama kati ya Moroko na jirani yake Algeria wampa mtihani kiongozi wa Ufaransa.

https://p.dw.com/p/CHBL
Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy.
Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy.Picha: AP

Itakua ziara ya kwanza nje ya bara la Ulaya, tangu alipochaguliwa kuwa Rais mwezi Mei mwaka huu. Hata hivyo kuna taarifa kwamba ziara ya Moroko imeahirishwa na sasa atazitembelea tu Algeria na Tunisia.

Rais Sarkozy alianza kupata mtihani huo wa ziara yake , baada ya Moroko kusema wiki iliopita kwamba siku mbili za ziara atakayoifanya Moroko hazitoshi, kabla ya taarifa kwamba imefutwa.

Maafisa wa kibalozi wamesema Moroko mshirika mkubwa na wa jadi wa Ufaransa inakerwa kuona kwamba Bw Sarkozy amepanga kuanza ziara yake Algeria, mpinzani wa Moroko katika kanda hiyo ya Afrika, na nchi ambayo ni nguvu ya nishati kutokana na akiba yake ya mafuta na gesi .

Mara kadhaa Moroko daima imekua kituo cha kwanza cha ziara zilizowahi kufanywa na marais wapya , pale walipochaguliwa viongozi wakuu waliopita wa Ufaransa. Kwa hivyo uamuzi wa Sarkozy wa kuanzia Algeria safari hii, unaangaliwa kama kosa na viongozi wa Moroko ambao wana uhusiano wa karibu na matangulizi wake Jacques Chirac na inaungwa mkono pia na Chirac katika mgogoro wake kuhusu Sahara magharibi, suala kuu la mvutano kati ya Moroko na Algeria.

Kader Abderahim, mtaalamu wa masuala ya nchi za maghreb-yaani Afrika kaskazini- katika taasisi ya uhusiano wa kimataifa mjini Paris, anaseama kuifuta ziara hiyo ya Rais Sarkozy ambaye ni mwanasiasa mwenye nguvu na maarufu miongoni mwa raia wa Ufaransa litakua kosa la kidiplomasia. Lakini akaongeza kwamba “Wamoroko walifikiria watakua na uhusiano na Sarkozy sawa na ule na Chirac, lakini hiki ni kizazi kingine na kipya katika siasa za Ufaransa”-hivyo mambo yanabadilika.

Wadadisi wanaashiria kwamba Sarkozy anaona hana deni lolote si kwa Moroko wala Algeria , lakini ukilinganisha nguvu za kibiashara, Algeraia ni dola yenye nguvu na muhimu. Sarkozy anataka kubadili muelekeo wa siasa za Ufaransa kuelekea Afrika ambayo anasema chini ya uongozi wa Chirac ulikua ni uhusiano wa kibinafsi kati ya viongozi.

Sarkozy anaelekea Algeria leo kwa mazungumzo na chakula cha mchana na Rais Abdelaziz Boutefliaka na baadae atakwenda Tunisia kuonana na Rais Zine al Abidine bin Ali. Ziara ndefu katika safari hiyo ilikua ile iliopangwa ni Moroko ambako angebakia kwa siku mbili.

Tunisia na Moroko ambazo zilikua himaya ya Ufaransa, ni maeneo makuu ya uwekezaji kwa Wafaransa, lakini Algeria ni mshirika mkubwa wa kibiashara katika Afrika.

Wakati wa ziara yake, inatarajiwa kwamba Rais Sarkozy atafafanua mpango wake wa kutaka kuwa na umoja wa mataifa ya bahari ya Mediterranean, ushirika kati ya nchi za kusini mwa ulaya na jirani zao wa Afrika kaskazini.

Lakini akiwa Algeria, Sarkozy hatarajiwi kubadili msimamo wa Ufaransa kuelekea Sahara magharibi. Mtangulizi wake Chirac aliiunga mkono Moroko katika pendekezo lake la kutaka mamlaka ya utawala katika ardhi hiyo ya wakaazi 260,000, wakati Algeria inakiunga mkono chama cha ukombozi wa Sahara magharibi Polisario chenye makao makuu nchini humo, katika dai lake kutaka pafanyike kura ya maoni juu ya mustakbali wa eneo hilo.

Tayari waziri mkuu wa zamani wa Algeria Redha Malek amenukuliwa akisema msimamo wa Sarkozy utatathiminiwa wakati wa ziara yake mjini Algiers. Kuahirishwa ziara yake Moroko, kunaonyesha jinsi suala hili lilivyo nyeti kwa Sarkozy.

Serikali ya Moroko haikutoa matamshi yoyote rasmi kuhusu kuahirishwa kwa ziara ya Kiongozi wa Ufaransa mjini Rabat, bali gazeti la “Al Massa” linalotoaka kila siku, liliandika kwamba “ Moroko inataka kumuona Sarkozy atakapokua na muda wa kutosha kuweza kujadiliana masuala yote yaliyo ya masilahi kwa nchi hizo mbili.