1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ziara ya siku tano ya waziri wa nje wa Marekani barani Ulaya

Oumilkher Hamidou12 Oktoba 2009

Hillary Clinton ashadidia umuhimu wa kutekelezwa makubaliano ya Ijumaa kuu huko Ireland ya kaskazini

https://p.dw.com/p/K4SP
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Hillary Clinton na waziri mwenzake wa Uengereza David MilibandPicha: AP

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani,Hillary Clinton anaendelea na ziara yake ya siku tano barani Ulaya.Ziara hiyo iliyoanzia Zurich Uswisi jumamosi iliyopita,imemfikisha London jana kabla ya kwenda Dublin na Belfast.Baadae leo usiku waziri huyo wa mambo ya nchi za nje wa Marekani anatazamiwa kwenda Moscow.

Iran na Afghanistan ndizo mada zilizogubika mazungumzo yake mijini Zurich ,London na Dublin na zinatarajiwa pia kujadiliwa waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani atakapokua ziarani mjini Moscow baadae leo usiku.

Lakini pia juhudi za amani katika Ireland ya kaskazini ambapo waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani anatazamiwa kupendekeza mchango mpya wa Marekani kusaidia kuukwamua mgogoro unaotishia utaratibu wa kugawana madaraka katika eneo hilo linalosimamiwa na Uengereza.Jana waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Hillary Clinton alikutana na waziri mkuu wa Uengereza Gordon Brown na waziri mwenzake wa Uengereza David Miliband aliyeyataja mazungumzo yao "kua ya kina,ya nguvu na ya maana."

Kuhusu suala la Afghanistan,waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani amesifu mchango wa vikosi vya Uengereza na kusema nchi zao mbili zinaendelea kuwajibika nchini Afghanistan.

Suala la Ireland ya kaskazini lilijadiliwa pia wakati wa mazungumzo yake pamoja na waziri mwenzake wa Uengereza David Miliband.Mazungumzo yao yalilenga juhudi za kufikia makubaliano ya kukabidhiwa madaraka pande zinazohusika.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Hillary clinton amesema:

"Nnaamini,kutokana na juhjudi za pamoja za serikali ya Uengereza,serikali ya Ireland,na uungaji mkono wa marafiki,ikiwa ni pamoja na Marekani,pande zinazohusika zitatanabahi hii ni hatua wanayobidi kuichukua kwa pamoja."

Hillary Clinton in Irland
Hillary Clinton akizungumza na mahasimu wawili wa Ireland ya kaskazini,McGuiness na RobinsonPicha: AP

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani alikwenda baadae Dublin kwa mazungumzo pamoja na waziri mkuu wa jamhuri ya Ireland Brian Cowen kabla ya kuelekea Belfast,jana usiku.

Hii leo waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani amekutana na viongozi wa makundi hasimu yanayounda serikali ya Ireland ya kaskazini huko Stormont,mashariki ya Belfast na kuwasihi wahakikishe ushirikiano kati ya wakatoliki na waprotestanti unaimarika.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani alikutana kwanza na waziri wa kwanza Peter Robinson na baadae na naibu waziri wa kwanza Martin McGuiness.

Robinson,ambae ni mprotestanti anapinga shinikizo la McGuiness na wakatoliki wengine wanaodai utawala wao ubebe jukumu la mfumo wa polisi na sheria katika Ireland ya kaskazini.

Serikali ya Uengereza,jamhuri ya Ireland na Marekani,kwa pamoja zinahisi hiyo ni hatua muhimu katika kuimarisha utaratibu wa kugawana madaraka-kitovu cha makubaliano ya amani yaliyofikiwa ijumaa kuu mwaka 1998.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Hillary Clinton anatazamiwa kuhutubia bunge la Ireland ya kaskazini baadae hii leo katika juhudi za kumaliza mvutano katika eneo hilo.

Mwandishi:Oummilkheir Hamidou(AFP/RTR)

Mhariri.M.Abdul-Rahman