1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jiabao atembelea Umoja wa Ulaya

Abdu Said Mtullya30 Januari 2009

China na Umoja wa Ulaya zaazimia kushirikiana katika kukabiliana na mgogoro wa fedha duniani.

https://p.dw.com/p/GkEF
Waziri Mkuu wa China Wen Jiabao akizungumza mjini Brussels.Picha: AP

China na Umoja  wa Ulaya zimekubaliana   kuitisha mkutano  wa viongozi wa pande hizo  haraka,  baada ya mkutano  uliopangwa  kufanyika hapo awali  kuahirishwa,  kutokana na kiongozi wa  kidini wa  Tibet  Dalai Lama kufanya  ziara katika nchi fulani  za Umoja  wa  Ulaya.

Rais wa  tume ya Umoja  wa Ulaya, Jose Manuel  Barosso, amesema hayo leo mjini Brussels baada  ya mazungmzo yake na waziri  mkuu wa China, Wen Jiabao,  anaefanya  ziara barani Ulaya.

Bwana Barosso amewaambia  waandishi habari  kwamba mkutano baina ya viongozi  wa  China na wa Umoja wa Ulaya  utafanyika haraka iwezekenavyo.

Bwana Barosso amesema kuwa Ulaya ina  dhamira kubwa katika kushirikiana na China.

Ziara ya waziri  mkuu wa China, Wen Jiabao, barani Ulaya ni ya kwanza kufanywa  na kiongozi  wa ngazi za  juu wa  China  tokea kuahirishwa  mkutano uliopangwa  kufanyika hapo  awali kutokana  na suala  la Dalai  Lama, kiongozi wa kidini wa Tibet  aliekutana na baadhi ya viongozi wa nchi  za Umoja wa Ulaya.Hatua hiyo iliikasirisha China  na iliamua  kuvunja  mkutano huo uliokuwa umepangwa  kufanyika mwezi Desemba mwaka jana.

 Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa alikuwa miongoni mwa viongozi  wa Ulaya waliokutana  na Dalai Lama.

Kwa mujibu wa China, Dalai Lama anaendesha  harakati zenye lengo la kulitenga jimbo la Tibet na China.

Akizungumzia  ziara  yake barani Ulaya, waziri mkuu wa China, Wen Jiabao, amesema kuwa  ziara hiyo imeinua hali ya kuaminiana na uelewano baina ya nchi yake na Umoja  wa  Ulaya.