1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zimbabwe yaahirisha mkutano wa COMESA

Mohamed Dahman13 Novemba 2008

Zimbabwe imeahirisha mkutano wa viongozi wa nchi wa jumuiya kubwa kabisa ya biashara barani Afrika COMESA ambao ulikuwa ukitarajiwa kuanzisha umoja wa forodha wa kanda hapo mwezi wa Desemba.

https://p.dw.com/p/FtrP
Rais Robert Mugabe, kushoto akipeana mkono na mpinzani wake mkuu Morgan Tsvangirai.Picha: AP

Zimbabwe ilikuwa inaandaa mkutano huo licha ya kwamba uchumi wake wenyewe ukiwa hoi na ikiwa kwenye mkwamo wa kugawana madaraka kati ya chama tawala cha ZANU- PF na kile cha upinzani cha MDC.

Zimbabwe ilikuwa imepanga kuandaa mkutano huo wa viongozi wa nchi katika Maporomoko ya Viktoria kujadili suala la kuimarisha biashara na kuboresha usalama wa chakula katika eneo zima la nchi za jumuiya hiyo ya COMESA juu ya kwamba uchumi wake wenyewe umesambaratika na takriban nusu ya watu wake wanahitaji msaada wa chakula wa dharura wa Umoja wa Mataifa.

Waziri wa biashara wa Zimbabwe Obert Mpofu ameliambia gazeti la serikali la The Herald kwamba sasa mkutano huo wa viongozi wa nchi wa jumuiya ya Soko la Pamoja la nchi za Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika COMESA utafanyika katika kipindi cha miezi sita ya kwanza ya mwaka 2009.

Mpofu amesema mkutano huo umeahirishwa ili kutowa muda zaidi kwa nchi wanachama 19 wa jumuiya hiyo kujadili kuoanisha ushuru ndani ya umoja wa forodha unaopangwa ambao ulikubaliwa nchini Kenya hapo mwaka jana.Mpofu amesema majadiliano yataendelea kupindukia tarehe 6 mwezi wa Desemba ambapo Umoja wa Forodha wa Jumuiya ya COMESA ulikuwa uzinduliwe.

Muda wa kufanyika kwa mkutano huo wa viongozi wa nchi ambao tayari umeahirishwa kutoka mwezi wa Mei unakuja wakati wa kipindi nyeti cha kisiasa kwa Zimbabwe baada ya uchaguzi tata wa rais kuiacha serikali ya nchi hiyo kwenye mkwamo na Zimbabwe yenyewe kwenye njia panda.

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe na kiongozi wa upinzani nchini humo Morgan Tsvangirai wamesaini makubaliano ya kugawana madaraka miezi miwili iliopita lakini mazungumzo hayo yamekwama kutokana mzozo wa jinsi ya kugawana nyadhifa muhimu za mawaziri.

Jumuiya ya ushirikiano wa maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika SADC katika mkutano wake wa vingozi wa nchi mjini Johannesburg Afrika Kusini hapo Jumapili iliopita ilitaka Mugabe na Tsvangirai kushirikiana udhibiti wa wizara ya mambo ya ndani wanayoigombania ambayo ndio yenye kusimamia polisi.

Mugabe wiki hii amesisitiza wamba ataunda serikali hivi karibuni licha ya pingamizi za Tsvangirai ambaye amemtuhumu kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 84 kwa kutaka kuuweka pembeni upinzani licha ya kuwa na viti vingi bungeni.

Mfarakano huo wa kisiasa umevunja mataumaini ya wananchi wa kawaida wa Zimbabwe kwamba harakati zao za kuendelea kuishi yumkini zikapunguwa makali.

Mataifa ya magharibi yamesema kwamba yako tyari kutowa mamilioni ya dola katika msaada lakini sio wakati Mugabe akiendelea kushikilia pekee hatamu za madaraka.