1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zimbabwe yakiuka itifaki ya kimataifa-Marekani

Kalyango Siraj6 Juni 2008

Polisi ya nchini humo yakanusha

https://p.dw.com/p/EEll
Mahasimu wawili wa kisiasa nchini Zimbabwe.Morgan Tsvangirai,kushoto,kiongozi wa chama cha upinzani cha Movement For Democratic Change -MDC na rais Robert Mugabe.Kuna madai kuwa wafuasi wa Mugabe wanawaandama wa Tsvangirai.Viongozi hao wawili watapambana tena katika duru ya pili ya uchaguzi wa urais itayofanyika katika kipindi cha wiki tatu zijazo.Uhusiano wa kiongozi wa MDC na mataifa ya magharibi yanazusha wasiwasi.Picha: AP

Polisi ya Zimbabwe imekanusha madai kuwa imekiuka itifaki ya kimataifa katika tukio moja dhidi ya mabalozi wa Marekani.

Na kwa wakati huohuo serikali ya Harare imesimamisha shughuli zote za utoaji wa misaada nchini humo,kwa kuyalaumu mashirika fulani kwa kujiingiza katika siasa za ndani ya nchi hiyo.

Hatua ya Polisi ya Zimbabwe kutoa taarifa leo ijumaa inayokanusha madai ya kwenda kinyume na itifaki ya kimataifa,ni alama ya kutokea mvutano mwingine kati ya serikali ya Harare na mataifa ya magharibi.

Na imefuatia malalamiko kutoka kwa serikali za Marekani na Uingereza zikitaka kupatiwa maelezo zaidi kwanini polisi ililizuilia kundi la mabalozi wa nchi za nje.

Mvutano ulianza jana alhamisi wakati kundi la wanadiplomasia wa ubalozi wa Marekani lilipokuwa linatembelea wilaya ya Bindura, inayopatikana umbali wa kilomita 100, kaskazini mashariki mwa mji mkuu wa Harare. Kundi hilo lilikuwa linachunguza taarifa zinazodai kutokea kwa ghasia na fujo dhidi ya wafuasi wa chama cha upinzani cha Movement for Democratic Change MDC.

Balozi wa Marekani James McGee amesema kuwa polisi ilijaribu kuwaamuru kwenda katika kituo cha polisi,jambo lilionekana kama kuwatia mbaroni,hii ikiwa kinyume na kinga ya kidiplomasia.

Balozi huyo ameongeza kuwa katika purukushani hiyo,polisi ilitoboa tairi za magari ya ubalozi na pia kuwa kundi la wapiganaji wa zamani liliwatishia kuwachoma moto wakiwa ndani ya magari yao.

Lakini msemaji wa polisi,Wayne Bvudzijena amenukuliwa na gazeti la serikali la Daily Herald, toleo la leo, akisema kuwa madiplomasia hao walikataa kujitambulisha waliposimamishwa na polisi. Afisa huyo ameongeza kuwa mabalozi hao walijaribu kutoroka na almanusura wawagonge maafisa wa polisi.

Aidha amesema kuwa mabalozi hao walijifungia ndani ya magari yao na hivyo kulazimisha maafisa wa polisi kutoa pumzi kutoka ndani ya matairi ya magari hayo. Ameongeza kuwa hali ilirudia kuwa ya kawaida baadae mabalozi hao walikubaliwa kuendelea mbele na safari yao.

Katika mazingira kama hayo polisi ya Zimbabwe pia imekanusha taarifa kuwa Morgan Tsvangirai alizuiliwa na polisi siku ya jumatano.

Tsvangirai ni kiongozi wa chama cha MDC na anamtia kishindo rais Mugabe katika duru ya pili ya uchaguzi wa urais. Afisa wa polisi akisema kuwa taarifa hizo ni za uongo,alifafanua kile anachosema kilichojiri.

Kwa muhatasari amesema kuwa kile polisi ilichokuwa inataka ni dereva aliekuwa nao kuwaeleza kuhusu makaratasi ya gari lake yaliyokuwa na dosari.

Badala yake magari ya Tsvangirai mengine yaliyokuwa yameruhusiwa kuendelea kuamua kwenda katika kituo kimoja cha polisi kilichokuwa karibu.

Na hayo yakiarifiwa mashirika ya kimisaada yanaonya kuwa hali ya raia wengi nchi humo iko mashakani kufuatia amri ya serikali ya kuyasimamisha kazi makundi ya utoaji msaada.Waziri mdogo wa habari wa Zimbabwe,Bright Matonga, ameliambia shirika la habari la AFP kuwa,mashirika hayo yamekuwa yakijihusisha katika shughuli za kisiasa.

Waziri wa huduma za jamii Nicholas Goche aliyaandikia mashirika hayo alhamisi akiyaamuru kusitisha shughuli za misaada nchini humo hadi yatakapoambiwa tena.

Kutafanyika duru ya pili ya uchaguzi wa urais nchini humo katika kipindi cha wiki tatu zijazo.Kiongozi wa upinzani Morgen Tsvangirai anatarajiwa kumbwaga rais Robert Mugabe na kuna wasiwasi kuwa huenda mashirika hayo yamekuwa yakimpigia debe Tsvangirai wakati yakigawa misaada.