1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zimbabwe yakubali kuwalipa fidia wakulima wazungu

30 Julai 2020

Serikali ya Zimbabwe imesaini makubaliano ya kulipa dola bilioni 3.5 za Kimarekani kama fidia kwa wakulima wazungu ambao ardhi yao ilichukuliwa na aliyekuwa rais marehemu Robert Mugabe.

https://p.dw.com/p/3gASj
Wakulima Zimbabwe
Picha: Reuters/P. Bulawayo

Rais Emmerson Mnangagwa amesema uamuzi huo umefanyika kwa mujibu wa katiba ili kufidia wakulima wazungu kwa hatua yao ya kuiboresha ardhi kwa kujenga mabwawa kabla ya ardhi hiyo kuchukuliwa kwa nguvu.

Kiongozi wa muungano wa kibiashara wa wakulima Andrew Pascoe ameonyesha kuridishwa na makubaliano hayo.

Pascoe ambaye muungano wake unajumuisha wakulima walionyang'anywa kwa nguvu ardhi yao katika miaka ya 2000 amesema na hapa amenukuliwa: "Baada ya karibu miaka 20 ya mzozo kuhusu suala la ardhi, wawakilishi wa wakulima waliopoteza ardhi kufuatia mageuzi ya sera za ardhi hatimaye wamekubaliana na wawakilishi wa serikali kumaliza mzozo huo. Kwangu mimi uamuzi huu ni kama miujiza.”

Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe
Picha: Getty Images/AFP/J. Njikizana

Makubaliano hayo yanaainisha kuwa asilimia 50 ya dola bilioni 3.5 italipwa katika muda wa miezi 12 huku fedha zilizosalia zikilipwa katika muda wa miaka mitano. Rais Mnangagwa amesema makubaliano hayo ni ya kihistoria kwani yanaashiria mwanzo mpya katika taifa hilo la kusini mwa Afrika.

Mnangagwa aliyeingia mamlakani mwaka 2017 baada ya Mugabe kulazimishwa kujiuzulu, amekuwa akiwahimiza wakulima wazungu kutuma maombi ya kumiliki baadhi ya vipande vya ardhi ili kuwekeza.

Wakulima wazungu walipoteza ardhi yao chini ya Mugabe

Afisa mmoja katika muungano huo wa kibiashara wa wakulima amesema zaidi ya wakulima 3,500 wametuma maombi ya kutaka kulipwa fidia.

Rais wa zamani wa Zimbabwe, Robert Mugabe
Picha: Espresso Media

Kulingana na makubaliano hayo, Zimbabwe itatoa dhamana za muda mrefu na pia itaunda timu inayojumuisha wakulima hao kuomba msaada zaidi kutoka kwa wafadhili wa kimataifa ili kupata fedha za kuwalipa fidia wakulima hao.

Wakulima wapatao 4,000 walipoteza ardhi yao kufuatia mageuzi yalioanzishwa na Hayati Robert Mugabe, ambayo mara nyingi yalikumbwa na vurugu, akitaja lengo lake kuwa ni kurekebisha ukosefu wa usawa wa enzi za ukoloni katika umiliki wa ardhi.

Wakulima wa kizungu walikuwa wanamiliki sehemu kubwa ya ardhi yenye rutuba ya kilimo. Hivi sasa ardhi ya kilimo inamilikiwa na serikali.