1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zoezi la kuhesabu kura laanza Tanzania

Tatu Karema
28 Oktoba 2020

Kazi ya kuhesabu kura na baadaye kujumlisha matokeo yake ndiyo inayoendelea sasa ikiwa yamepita masaa mawili tangu milango katika vituo vya kupigia kura iliyofunguliwa tangu saa moja asubuhi ifungwe kuanzia sasa kumi.

https://p.dw.com/p/3kYN9
Tansania | Präsidentschaftswahlen
Picha: Ericky Boniphace/DW

Vituo vya kupigia kura katika uchaguzi mkuu wa Tanzania vimefungwa tangu saa kumi jioni huku tume ya taifa ya uchaguzi NEC ikisema kata nne hazijafanya uchaguzi wa madiwani kutokana na sababu mbalimbali.

Na muda mchache uliopita, mwenyekiti wa tume ya taifa ya uchaguzi NEC, Jaji Mstaafu, Semistocles Kaijage ametoa taarifa ya awali kuhusu mwenendo wa uchaguzi akitaja pia kata nne zilishindwa kufanya uchaguzi wa ngazi ya madiwani kutokana na sababu kuu mbili. Mosi amesema kuwa kata tatu hazikufanya uchaguzi huo baada ya wagombea wake kufariki dunia huku kata moja uchaguzi huo ukibidi uahirishwe baada ya kukosekana kwa karatasi za kupigia kura. Mwenyekiti huyo amesema kata hizo zitafanya uchaguzi wake katika muda utakaotangazwa hapo baadaye.

Kumekuwa na ripoti kuhusu kuwepo kwa baadhi ya kura bandia katika baadhi ya vituo na nyingi za ripoti hizo zinasema kura hizo zilikamatwa katika jimbo la Kawe jijini Dar es salaam, Pangani Tanga na Buhigwe huko Kigoma. Hata hivyo, mwenyekiti huyo wa tume amesema ripoti hizo hazijabainisha bayana ni vituo vipi kura hizo zilikamatwa na wala tume hiyo haijathibitisha kuhusu madai hayo.

Tansania | Präsidentschaftswahlen
Mpiga kura awasilisha kura yakePicha: Ericky Boniphace/DW

Katika tukio hilohilo la kuwepo kwa kura bandia, mgombea ubunge wa chadema katika jimbo la Kawe, Halima Mdee ameachiwa na jeshi la polisi baada ya kushikiliwa kwa muda kutokana na tafrani iliyojitokeza kuhusiana na suala hilo. Wafuasi wa chama hicho waliokuwepo katika moja ya kituo cha kupigia kura walidai kuwabaini baadhi ya watu wakiwa na kura hizo hali iliyosababisha kuwepo kwa vuta nikuvute. Baadaye picha za video zilionyesha namna wafuasi hao wakizichoma moto zinazodaiwa kuwa kura hizo bandia.

Kwa upande mwingine kuendelea kubinywa kwa mitandao ya mawasiliano kama vile internet iliyopunguzwa kiwango chake kumesababisha kilio kikubwa kwa mamia ya wananchi wanaosema wanashangazwa na kitendo hicho wanachodai kinajitokeza kwa mara ya kwanza katika historia ya kurejea kwa uchaguzi wa mfumo wa vyama vingi tangu mwaka 1995. Kumekuwa na shida ya kupata mawasiliano ya internet huku baadhi ya huduma kama whatsapp, you tube, twiter na mitandao mingine ikisitishwa kabisa. Hii ni mara ya kwanza kwa hali kama hiyo kushuhudiwa nchini.