1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zu Guttenmberg Marekani

17 Machi 2009

Waziri wa uchumi wa Ujerumani amezungumza na wakuu wa General Motors juu ya hatima ya OPEL

https://p.dw.com/p/HE3Y
Karl-Theodor zu GuttenbergPicha: picture-alliance / dpa

Baada ya mazungumzo yake na wakuu wa Banki mbali mbali za Marekani mjini New York, waziri wa uchumi wa Ujerumani, Karl-Theodor zu Guttenberg, alikutana jana jioni mjini Washington na uongozi wa kiwanda kikubwa kabisa cha magari-GENERAL MOTORS. Mazungumzo yao ya kiasi cha saa 2 yalilenga kutafuta ufumbuzi wa kuliokoa tawi la General Motors - kampuni la OPEL .

Baadhi ya wakati akizungumza wazi wazi na wakati mwengine kwa mafumbo, waziri wa uchumi wa Ujerumani, Karl-Theodor zu Guttenmberg, akimkaripia meneja wa viwanda vya magari vya General Motors na Opel. Kwani amegundua kwamba mkakati wa kulirekebisha kabisa na kuliimarisha kampuni hilo si imara na haujibu baadhi ya maswali muhimu.

Baada ya mkutano wake na mkuu wa kampuni la magari la General motors, Rick Wagoner huko Washington, Bw. zu Guttenberg, ameibuka mwenye matumaini zaidi. Kwani ameona kampuni la General Motors yadhihirika sasa liko tayari kuliachia tawi lake la kiwanda cha OPEL nchini Ujerumani kujiendesha wenyewe bila ya kuliingilia. Na baada ya mazungumzo hayo, Bw. Zu Guttenberg alisema General motors, kimsingi, liko tayari kuachia haki zake miliki katika kampuni la magari la OPEL.Kwa muda mrefu haki hizo zilikuwa mikononi mwa serikali ya Marekani. Zilihifadhiwa huko kama dhamana kwa msaada uliotolewa na serikali kwa kampuni hilo.

"Tulizusha swali la hati-miliki na General Motors likaonesha liko tayari, kimsingi, kuachana na haki hizo. Halafu tukauliza iwapo General Motors ingeridhia kuwa na hisa ndogo tu huku Ulaya. Na katika hili pia liko tayari, kimsingi, kuridhia.Tuliuliza pia iwapo GM itayari hisa hizo kuziachia na hata juu ya swali hilo GM iko tayari. Iliobakia sasa ni iwapo serikali ya Marekani nayo pia inaridhia hayo ."

Sasa ili kupata ufafanuzi zaidi, anaweka matumaini katika mazungumzo yake ya leo na waziri wa fedha wa Marekani, Timothy Geithner.Kuhusu wasi wasi na hofu walizonazo wafanyikazi wa kiwanda cha Opel, zu Guttenberg aliwaambia kwamba jioni ya jana ilikuwa wakati ambao haukutukatia matumaini.

Hata hivyo, aliongeza shida bado zimesalia katika kumpata mtiaji-raslimali wa kibinafsi. Kutokana na msukosuko wa sasa wa fedha, mara kwa mara kidole kinanyoshewa kuwapo kwa wafanyikazi wengi kupita kiasi katika kiwanda hiki cha kutengeneza magari. Si ajabu, kwa hivyo, kuona hakuna ambae yuko tayari kwa sasa kutia raslimali yake katika sekta hii ya kiwanda. Waziri wa uchumi wa Ujerumani, hata hivyo, anaendelea kujitahidi kusaka waekezaji katika kiwanda cha Opel.

Mwandishi: Jenter, Steffen/Ali, Ramadhan/ZR

Mhariri: Miraji Othman