1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zuma ambwaga Mbeki kwenye uongozi wa ANC Afrika Kusini

19 Desemba 2007
https://p.dw.com/p/CdUj

POLOKWANE

Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini hapo jana ameangushwa kwa idhara kutoka hatamu za uongozi wa chama tawala nchini humo cha ANC na mpizani wake Jacob Zuma ambaye alimtimuwa kwenye wadhifa wa makamo wa rais miaka miwili iliopita.

Baada ya mchuano mkali wa uchaguzi huo ambao pia umeshuhudia wasaidizi wakuu wa Mbeki wakipoteza nyadhifa zao kwenye chama hicho Zuma alitangazwa rasmi kuwa mshindi baada ya kusomba takriban asilimia 60 ya kura.

Dren Nupen mkuu wa tume ya uchaguzi ya chama akitangaza ushindi wa Zuma amesema amejizolea kura 2,329 wakati Mbeki aliekuwa akitetea wadhifa wake wa urais wa chama amejipataia kura 1,505.

Wakati ushindi huo ukitangazwa Mbeki alimkumbatia Zuma huku kukiwepo hoi hoi za kushangilia.

Ushindi huo unaashiria kurudi kwa vishindo kwenye jukwaa la kisiasa kwa Zuma ambaye bado anakabiliwa na madai ya rushwa. Kutokana na ushindi huo wa Zuma mamlaka ya Mbeki itakuwa imedhoofika kwa vile bado ana miaka miwili ya kubakia kwenye madaraka ya urais kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2009.

Zuma mwenye umri wa miaka 65 alitimuliwa kwenye wadhifa wa makamo wa rais na Mbeki hapo mwaka 2005 wakati mshauri wake wa kifedha alipofungwa kutokana na hujuma.Baadae Zuma alishtakiwa kwa kumbaka mwanamke rafiki wa familia ambaye amempita kwa umri maradufu.

Juu ya kwamba Zuma alionekana kuwa hana hatia katika kesi hiyo alidharaulika sana kwa kutowa ushahidi kwamba alifanya mapenzi na mwanamke huyo mwenye virusi vya UKIMWI kwa ridhaa yake na kwamba alikwenda kukoga baadae ili kuzuwiya maambukizi ya virusi hivyo.

Kwa kuzingatia kwamba chama cha ANC kina wingi wa viti bungeni Zuma moja kwa moja anahakikishiwa kuwa rais wa taifa katika uchaguzi wa mwaka 2009 ili mradi anashinda katika madai ya rushwa yanayomkabili.

Uhasama kati ya Mbeki na Zuma umesababisha mgawanyiko mkubwa ndani ya chama wakati wa wa mkutano wake mkuu unaofanyika kwenye mji wa kaskazini wa Polokwane ambao unamalizika hapo kesho Alhamisi.