1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zuma aweza shtakiwa kwa tuhuma za rushwa.

Halima Nyanza20 Desemba 2007

Kiongozi mpya aliyechaguliwa wa chama tawala cha Afrika Kusini –ANC- Jacob Zuma, ambaye atatarajiwa pia kuwa Rais wa nchi hiyo baadaye, matarajio hayo yanaweza kukwamishwa, kutokana na tuhuma za rushwa zinazomkabili.

https://p.dw.com/p/CeHi
Mwenyekiti mpya wa chama tawala nchini Afrika kusini, Jacob Zuma, ambaye kwa sasa anaweza kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za rushwa.Picha: AP

Si zaidi ya siku mbili tangu Jacob Zuma kupata ushindi katika uchaguzi uliokuwa ukifatiliwa kwa ukaribu zaidi sehemu mbalimbali duniani, wa kiongozi wa juu wa chama tawala cha Afrika kusini cha ANC, uchaguzi ambao uliweza kumuangusha mpinzani wake, Rais wa nchi hiyo Thabo Mbeki, Kaimu Mwendesha mashtaka mkuu wa nchi hiyo Mokotedi Mpshe amesema kuna ushahidi wa kutosha kumshtaki Bwana Zuma baada ya kukamilisha uchunguzi wa tuhuma za rushwa dhidi yake.

Amesisitiza kuwa wanaushahidi wa kutosha kuweza kufungua kesi mahakamani na kwamba kesi itafunguliwa karibuni.

Mshauri wa Jacob Zuma katika masuala ya fedha Schabir Saik kwa sasa anatumia kifungo cha miaka 15 gerezani baada ya kukutwa na hatia ya kuomba rushwa kwa niaba ya mwenyekiti huyo mpya wa ANC.

Mashtaka hayo yanamhusisha Zuma na kashfa ya ununuzi wa silaha, ambapo anadaiwa kukubali rushwa ya karibu dola laki sita kwa kampuni moja ya silaha ya Ufaransa.

Tuhuma zilizokuwa zikimkabili awali Jacob Zuma ziliondolewa baada ya Jaji kutupilia mbali kutokana na kutokuwepo kwa ushahidi wa kumshtaki, lakini hata hivyo serikali ya nchi hiyo ili endelea kuchunguza tuhuma hizo.

Tuhuma hizo za rushwa zilizoibuka upya, zimeelezwa kuwa ni kutaka kuutia dosari ushindi alioupata Bwana Zuma.

Mwenyekiti wa Jumuia ya Vijana wa ANC Fikile Mbalula, amesema kuwa shutuma dhidi ya kiongozi wao huyo mpya sio ngeni masikioni mwao na kamba kamwe hazitabadili mwelekeo wao: ’’Bila ya shaka jambo la kwanza na la muhimu, haijawahi kutokea katika historia ya utendaji haki kwa mtu akiwa na kesi kwanza mtangaze katika vyombo vya habari. Hiki ni kitu ambacho mtu anatakiwa kukifanya kwanza kiutawala kwa kufuata taratibu za kisheria. Na kwamba taarifa hiyo siyo mpya, na sio kitu ambacho kitabadili mioyo yetu. Ni kitu ambacho tulikuwa tukikitarajia kwa sababu Jacob Zuma amekuwa akipakwa matope kwa mwaka mzima na hiyo sio njia nzuri ya kumtendea mtu haki yake.’’

Naye mweka hazina mpya wa chama hicho ambaye yuko upande wa Bwana Zuma Mathes Phosa anasema shutuma hizo zinazomwandama kiongozi wao mpya zimetengenezwa na kikosi cha polisi nchini humo maarufu kama n’nge.

Hata hivyo amesema haelewi kwanini, Kaimu mwendesha mashtaka mkuu wa serikali ya nchi hiyo amezivujisha taarifa kwa vyombo vya habari na kueleza kuwa kitendo hicho ni cha kumzalilisha Bwana Zuma.

Mbali na shutuma za rushwa, kiongozi huyo mpya wa Afrika kusini pia amewahi kuponea chupuchupu na mashtaka mengine ya ubakaji yaliyokuwa yakimkabili.

Kwa kushinda nafasi hiyo ya uenyekiti wa ANC, baada ya kuchaguliwa siku ya Jumanne usiku ya wiki hii, Jacob Zuma mwenye umri wa miaka 65 amejiweka katika nafasi nzuri ya kuwa mrithi wa Rais Mbeki katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2009.