1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zuma kung'olewa au kunusurika

Sylvia Mwehozi
8 Agosti 2017

Wabunge wa Afrika Kusini mchana huu, watapiga kura ya siri ya kutokuwa na imani na Rais Jacob Zuma, kura ambayo itakuwa ya siri na hivyo kuwepo na mwanya  wa kiongozi huyo mwenye miaka 75 kuondolewa madarakani. 

https://p.dw.com/p/2hs60
Südafrika Präsident Jacob Zuma
Picha: Reuters/P. Bulawayo

Tangu majira ya asubuhi, waandamanaji wameanza kukusanyika katika mitaa ya mji wa Cape Town eneo liliüp jengo la bunge la Afrika Kusini, huku wakiwa wamebeba mabango ya kuwataka wabunge kumfuta kazi Zuma. Mabasi makubwa yaliyowabeba wafuasi wa upinzani yalimiminika katika mji huo na kusababisha msongamano mkubwa.

Mmusi Maimane aliye kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha Democratic Alliance, DA, alitarajiwa kuhutubia umati mkubwa uliokusanyika nje ya bunge, lakini hapo jana alitoa rai ifuatayo, "kesho kuchagua ni rahisi sana, ni kuchagua kama unasimama na Jacob Zuma au unampinga, ni rahisi sana kama hivyo. Unasimama kwa ajili ya maslahi ya Afrika Kusini au sio." Maafisa wa polisi nao wameendelea na doria katika mitaa na barabara zinazoingia katika eneo la bunge.

Zuma amenusurika mara saba katika kura ya kutokuwa na imani naye tangu awe rais mwaka 2009. Lakini kura hizo mara zote zimekuwa za wazi na hivyo kuwalazimisha wanachama wa chama tawala cha African National Congress, ANC, kutii masharti ya chama.

Südafrika Kommunalwahl Oppostion Mmusi Maimane
kiongozi wa chama cha Democratic Alliance Mmusi MaimanePicha: picture-alliance/AP Photo/H. Verwey

Vyama 9 kati ya vyama vyote 13 vilipendekeza kura ya siri, ambayo kwa mara ya kwanza itawaruhusu wanachama wa chama cha Zuma ambacho kimegawanyika, kupiga kura bila ya hofu ya kulipiziwa kisasi. Ili bunge liweze kumuondoa Zuma, kutahitajika angalau kura 50 za kumpinga kutoka wabunge 249 wa ANC, ukiongeza na nyingine za wabunge wa upinzani katika bunge lenye viti 400. Ikiwa ndivyo, rais na baraza lake watalazimika kujiuzulu, na kuruhusu bunge kumchagua rais mpya miongoni mwa wanachama wake au kuitisha uchaguzi wa mapema.

Kura ya kutokuwa na imani na rais ilipendekezwa na chama cha DA mwezi Aprili baada ya Zuma kumfuta kazi waziri wa fedha anayeheshimika, Pravin Gorghan, na kuyafanya makampuni mawili ya viwango kushusha uwezo wa Afrika Kusini kukopesheka kwa kiwango cha chini.

Kushushwa huko kulifuatia mfululizo wa kashfa za rushwa na Zuma menyewe amekuwa kikangooni kwa namna ameshughulikia suala la uchumi. Karibu asilimia 28 ya nguvu kazi nchini humo haina ajira, kwa mujibu wa takwimi zilizotolewa Jumatatu.

Wakosoaji wa Zuma wanamuona kama mtu aliyekiua chama cha ANC ambacho kiliongoza harakati za ukombozi na kuitawala Afrika Kusini tangu kuchaguliwa kwa Nelson Mandela kama rais wa kwanza aliyepatikana kidemokrasia na aliyehitimisha utawala wa kibaguzi mwaka 1994.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/dpa

Mhariri: Mohammed Khelef