1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ABIDJAN: Vikosi vya amani vyatuhumiwa ukiukaji wa kijinsia

21 Julai 2007
https://p.dw.com/p/CBgU

Kundi moja la vikosi vya amani vya Umoja wa Mataifa nchini Ivory Coast,limeamriwa na Umoja wa Mataifa kubakia kambini.Hatua hiyo imechukuliwa baada ya Umoja wa Mataifa kupokea malalamiko yanayohusika na ukiukaji wa kijinsia.Hayo ni malalamiko mapya katika orodha ndefu ya tuhuma za aina hiyo,dhidi ya vikosi vya amani vya Umoja wa Mataifa,sehemu mbali mbali duniani.

Msemaji rasmi wa Umoja wa Mataifa hakutaja ni wanajeshi wa nchi gani waliohusika,lakini kwa mujibu wa wanadiplomasia na maafisa,kama walinzi wa amani 800 wa Morocco wamesitishwa kazi,baada ya uchunguzi wa ndani kugundua kuwa mamia kadhaa ya wanajeshi hao,walihusika na ngono pamoja na wasichana wenye umri mdogo.Umoja wa Mataifa umesema,hautostahmilia hata kidogo vitendo vya aina hiyo.

Kwa mujibu wa maafisa wa Umoja wa Mataifa,katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita,zaidi ya wanajeshi wake 300 sehemu mbali mbali duniani, wamefanyiwa uchunguzi kuhusika na udhalilishaji wa kijinsia.Madai yanapothibitishwa,wakosaji hurejeshwa makwao ikitumainiwa kuwa serikali zao zitawashtaki kuambatana na makubaliano yaliyokuwepo kati ya Umoja wa Mataifa na nchi zinazochangia vikosi vya amani.Lakini hadi hivi sasa,ni nchi chache sana zilizoripotiwa kufungua kesi zinazohusika na mashtaka ya aina hiyo.