1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ACCRA: Mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika wamalizika

4 Julai 2007
https://p.dw.com/p/CBm4

Mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika ulimalizika jana usiku mjini Accra Ghana bila kufikia makubaliano ya kuunda serikali moja ya bara la Afrika.

Viongozi waliohudhuria mkutano huo hawakuweka tarehe ya kuundwa kwa serikali hiyo baada ya tofauti kubwa kuzuka miongoni mwao.

Hata hivyo viongozi hao walikubaliana kuanzisha uchunguzi kutathmini vipi na lini serikali ya Umoja wa Afrika itakapoweza kuundwa.

Matokeo ya uchunguzi huo yanatarajiwa kuwasilishwa kwa kamati ya viongozi wa nchi. Akizungumza mwishoni mwa mkutano huo wa siku tatu, rais wa Ghana, John Kufuor, alisema viongozi hao wanatarajiwa kuwasilisha mapendekezo yao kwenye mkutano mwingine uliopangwa kufanyika mwezi Januari mwaka ujao.

Kushindwa kwa mkutano wa mjini Accra kufikia makubaliano ni pigo kubwa kwa rais Muammar Gaddafi wa Libya na rais wa Senegal, Abdoulaye Wade, ambao waliunga mkono kwa dhati kuundwa kwa serikali ya bara la Afrika.