1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ADDIS ABABA: Serikali ya Sudan imekubali kikosi cha kijeshi cha Umoja wa mataifa na Umoja wa Afrika

17 Novemba 2006
https://p.dw.com/p/CCrr

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Kofi Annan, amesema serikali ya Sudan imekubali kimsingi kupelekwe kikosi cha mchanganyiko wa wanajeshi kutoka Umoja wa mataifa na Umoja wa Afrika katika jimbo lenye machafuko la Darfur, magharibi mwa Sudan. Hadi sasa serikali ya Sudan inapinga kikosi cha kijeshi cha Umoja wa mataifa pekee yake. Kofi Annan, ameyasema hayo baada ya mazungumzo juu ya mzozo wa Darfur, yaliyofanyika mjini Addis Ababa nchini Ethiopia. Lakini wawakilishi wa serikali ya Sudan wamesema wanahitaji kushauriana na viongozi wao kabla ya kutoa kibali cha mwisho. Annan amesema kikosi hicho kitaweza kuwa na wanajeshi 27,000.

Bibi Marina Peters wa mtandao unaoshughulikia maswala ya Sudan, ´´Sudan Focal Point Europe´´, anasema bado kuna hatua kubwa ya kupigwa:

´´Kinachohitajika ni mchakato wa kuleta maridhiano miongoni mwa wananchi wote. Kwani bado wamegawanyika sana. Kadhalika katika makundi ya waasi pia, pana migawanyiko. Awali ya yote, tunahitaji suluhisho juu ya wanamgambo wa Janjawid ambao hasa ndiwo wanasababisha umwagaji damu´´

Kulingana na makisio ya Umoja wa mataifa, watu laki mbili wameshauawa na wengine takriban milioni 2 kuyahama maskani yao tokea kuzuka mzozo huo wa Darfur miaka mitatu iliopita.