1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

AFCON: Ghana walazimisha sare ya 2-2 na Misri

Mohammed Khelef
19 Januari 2024

Ghana imefanikiwa kulazimisha sare ya mbili kwa mbili na kinara wa soka ya Afrika, Misri, katika mechi ya usiku wa Alkhamis, baada ya Mohammed Kudus kuyaweka kimiani magoli yote mawili ya Nyota hao Weusi.

https://p.dw.com/p/4bRDd
AFCON 2024 I Misri vs Ghana
Mechi ya Ghana na Misri kwenye michuano ya AFCON 2024 nchini Ivory Coast.Picha: Kim Price/Newscom/picture alliance

Matumaini ya Misri kuendeleza rikodi yake ya kulitwaa Kombe la Afrika kwa mara ya nane yalipata pigo kabla ya kumalizika kwa kipindi cha kwanza, pale nyota wake, Mohamed Salah, alipolazimika kutoka nje kutokana na majeraha kwenye mguu wake wa kushoto.

Kocha wake, Rui Vitoria, alisema bado ni mapema kusema ikiwa Salah ataweza kuendelea na mechi nyengine zilizosalia kwenye michuano hiyo. Kocha huyo aliyaita matokeo ya jana kuwa mabaya, ingawa alisema wana uhakika wa kurudi na kombe nyumbani.

Kwa upande wake, kocha wa Ghana, Chris Hughton, alisema ameridhishwa na kiwango walichokionesha wachezaji wake, ambacho kama wakikiendeleza kwenye mechi ya Jumatatu na Msumbiji, wanaweza kuvuuka duru hii ya mtoano na kuwa mojawapo ya timu mbili za Kundi B kusonga mbele.

Hata hivyo, bado matokeo hayo yanaiweka Ghana mkiani kwenye Kundi hilo, sambamba na Msumbiji yenye pointi moja, huku Misri ikiwa ya pili kwa pointi mbili nyuma ya kiongozi wa kundi hilo, Cape Verde, yenye pointi 3.

AFCON2024 I Misri vs Ghana
Mohamed Salah wa Misri kabla ya kuumia na kutoka nje kwenye mechi na Ghana siku ya Alkhamis (Januari 18).Picha: Ulrik Pedersen/DeFodi Images/picture alliance

Katika mechi za Ijuma (Januari 19), Cape Verde itakwaana na Msumbiji kwenye mechi zao za pili katika michuano hiyo ya AFCON. 

Katika mechi za kwanza, Cape Verde iliibwaga Ghana 2 kwa 1 huku Msumbiji ikitoka sare ya mbili kwa mbili na Misri siku ya Jumapili. 

Soma zaidi: Raundi ya pili ya mechi za makundi kuanza AFCON

Senegal iliyoibwaga Gambia kwa mabao matatu kwa nunge kwenye mchezo wa awali, siku ya Ijumaa ilitatazamiwa kuumana Cameroon, ambayo kwenye mchezo wake wa kwanza ilitoka suluhu ya moja kwa moja na Guinea. 

Guinea nayo ilitarajiwa kukumbana na Gambia, zote mbili zikiwania kusalia kwenye Kundi C, linaloongozwa na Senegal yenye pointi tatu. 

Timu mbili tu kwa kila kundi ndizo zenye fursa ya kusonga mbele.

Nigeria yailaza Ivory Coast 1-0

Katika mechi za Kundi A siku ya Alkhamis, Nigeria iliwabwaga wenyeji wa michuano hiyo, Ivory Coast, kwa bao moja bila, lililowekwa wavuni kwa mkwaju wa penalti wa William Troost-Ekong katika kipindi cha pili.

Tai hao wa Nigeria walicheza wakiwa na shinikizo la kushinda mechi yao hiyo baada ya kulazimishwa suluhu ya moja kwa moja kwenye mchezo wa ufunguzi na Guinea ya Ikweta hapo Jumapili. 

Ivory Coast | Africa Cup of Nations | CIV vs. Nigeria
William Troost-Ekong wa Nigeria (katikati) akishangiria bao lake dhidi ya Ivory Coast siku ya Alkhamis (Januari 18).Picha: Franck Fife/AFP

Ikiwa na pointi nne kibindoni, kwa sasa Nigeria imejihakikishia kuvuuka awamu hii ya mtoano na kusonga mbele kwenye duru ya pili.

Soma zaidi: Moroko yaichabanga Tanzania 3-0 AFCON

Kwenye mechi nyengine ya Kundi hilo la A hapo jana, Guinea ya Ikweta iliilaza Guinea-Bissau nne - mbili, kinara wa mchezo akiwa Emilio Nsue aliyefunga bao kwa hat trick. 

Nsue, mwenye umri wa miaka 34 amekuwa mchezaji mwenye umri mkubwa kabisa kufunga kwa staili hiyo katika michuano hii ya AFCON mwaka huu na wa kwanza kwa miaka 16 iliyopita. Mchezaji wa mwisho kufanya hivyo alikuwa Soufiane Alloudi wa Moroko mwaka 2008. 

Kwa matokeo haya, Guinea ya Ikweta ndiyo inayoongoza Kundi A sambamba na Nigeria, zote zikiwa na pointi 4 kila mmoja. 

Guinea ya Ikweta itavaana na wenyeji Ivory Coast hapo Jumatatu, huku Nigeria ikichuana na Guinea-Bissau, kwenye mechi za uamuzi wa timu gani mbili zitakazosonga mbele kwenye duru ya pili.