1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika kutawala katika mkutano ujao wa Viongozi wa nchi zilizoendelea kiviwanda duniani

Mohammed Abdul-Rahman14 Mei 2007

Kansela Angela Merkel aahidi kulipigia debe bara hilo, ili ahadi zilizotolewa zitekelezwe.

https://p.dw.com/p/CHER
Kansela Merkel akiwa na mwana harakati na muimnbaji Bono (kushoto) wa kundi la U2 mjini Berlin
Kansela Merkel akiwa na mwana harakati na muimnbaji Bono (kushoto) wa kundi la U2 mjini BerlinPicha: AP

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ameahidi kulipa msukumo suala la Afrika na matatizo inayoyakabili, katika mkutano wa kilele wa nchi zilizoendelea kiviwanda, kundi linalojulikana kama G8 , akisema hilo si bara lililoachwa mkono. Tangazo la Kansela lilitolewa kwa njia ya mtandao wa Internet, likihusika hasa na Afrika,ambapo amewataka viongozi wakuu wa mataifa ya G8 watimize ahadi zilizotolewa awali kuhusu nyongeza ya msaada wa fedha kwa bara la Afrika. Mohammed Abdul-Rahman anayo zaidi.

Kansela Angela Merkel amelisogeza suala jengine zito katika jukwaa la mkutano huo wa kilele wa mataifa yalioendelea kiviwanda duniani utakaofanyika majuma manne yajayo hapa Ujerumani. Mbali na suala la mabadiliko ya hali ya hewa na takawa la kuwepo na uwazi zaidi katika masoko ya fedha, Bibi Merkel anakusudia kuwashinikiza viongozi wa mataifa yanayounda kundi hilo la G8 wachukua hatua za kivitendo kupambana na majanga katika Afrika.

Katika taarifa yake ya kila wiki kupitia mtandao wa Internet, Kansela alisema mataifa tajiri duniani yanaweza kuleta mabadiliko. Kushindwa kulisaidia bara la Afrika alisema, kunakua na athari katika nchi za viwanda. Moja kati ya matatizo hayo ni wimbi la wakimbizi. Bibi Merkel akasema ,“Kama hatutajali juu ya hatima ya majirani zetu katika ulimwengu huu wa utandawazi, siku moja tutayaona matatizo yakiwa mlangoni mwetu. Uhamiaji wa wakimbizi unaweza tu kuzuiwa ikiwa tutaweza kulitatua tatizo hili katika nchi zao. Na lazima tufanye hivyo sasa. “

Katika risala yake hiyo Kansela wa Ujerumani alielezea suala la kupunguzwa mzigo wa madeni, na kuongezwa msaada wa maendeleo kwa Afrika kuwa masuala ya msingi katika ajenda ya mkutano wa G8. Kadhalika alisema vita dhidi ya ukimwi na magonjwa mengine yakuambukiza kuwa changa moto kubwa inayohitaji kushughulikiwa haraka. Bibi Merkel akawataka viongozi wa nchi za kiafrika, wajitolee katika kuhakikisha kuna utawala bora na taasisi imara-hayo yakitajwa kuwa masharti makuu ya maendeleo.

Wakati huo huo jumuiya za kimataifa zisizokua za kiserikali na makundi yanayoendesha kampeni ya kulitetea bara la Afrika, yanaimarisha mbinyo wao kwa Kansela. Bono, muimbaji maarufu wa bendi ya muziki ya Uingereza U2, jana alikutana na viongozi wakisiasa wa Ujerumani akiwaambia kwamba dunia ina matarajio makubwa kutokana na wenyekiti wa Ujerumani wa kundi hilo la mataifa yalioendelea kiviwanda G8 ,akisema “Tunashukuru sana kwamba ni Ujerumani ambayo tunahisi itatimiza ahadi yake. Tunaiangalia Ujerumani kama nchi isiyovunja miadi . Na tunajua kwamba tuna uungaji mkono wenu katika kujaribu kuyapitisha yale yanayoonekana kuwa ni matatizo katika kufafanua fikra hizi.”

Wanaharakati wanakosoa kwamba msaada rasmi wa maendeleo kwa Afrika uliongezeka tu kwa mbili asili mia katika 2006. Bono anasema hali hii ni kinyume kabisa na ahadi za viongozi wa G8 wakati wa mkutano wao wa kilele nchini Scotland 2005, ambapo waliahidi kuongeza maradufu msaada kwa Afrika katika kipindi cha miaka mitano ijayo. Katika mkutano huo pia mataifa tajiri duniani yakaahidi kuongeza msaada jumla wa maendeleo kwa 0.7 asili mia ya pato lao jumla la taifa, jambo ambalo nchi zote zimeshindwa kulitimiza.

Muimbaji huyo wa kundi la muziki la U2 anasema hadi ahadi hizo zitakapotimizwa, wanaharakati wataendelea kumkumbusha Kansela Merkel na viongozi wenzake juu ya ahadi zao. Akaongeza ,“Tutakua katika mwezi mzima ujao tukiwapa shinikizo. Nina hakika. Lakini nafikiri ni kazi yetu na najua mnaiheshimu.”

Mkutano huo wa Viongozi wakuu wa taifa na serikali wa nchi 8 zilizoendelea kiviwanda duniani, utafanyika Juni 6 hadi 8 katika mji wa Ujerumani wa Heiligendamm.