1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika yageuzwa jalala la taka za kielektroniki

Saumu Ramadhani Yusuf10 Novemba 2010

Ingawa teknolojia ya vifaa vya mawasiliano imekuwa ikiisaidia Afrika, sasa bara hili masikini linakabiliwa na hatari ya kugeuzwa jalala la vifaa vikuukuu kutoka Ughaibuni na hivyo kutishia usalama wa mazingira

https://p.dw.com/p/Q3gu
Vijana wa Kimaasai wakitupia kompyuta ya mkononi kupata taarifa
Vijana wa Kimaasai wakitupia kompyuta ya mkononi kupata taarifaPicha: CORBIS

Teknolojia ya mawasiliano kama vile kompyuta, simu za mkononi na kadhalika zina manufaa yake mengi barani Afrika. Lakini madhara yake ni pale vinapoingizwa vifaa ambavyo ni vikuukuu na havichukui muda kuharibika na kushindwa kabisa kufanyakazi.

Shrika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Mazingira (UNEP) limetoa wito kwa mataifa ya Afrika kuchukua hatua madhubuti kukabiliana na ongezeko kubwa la kuingizwa barani humo kwa vifaa hivyo vya elektroniki.

Computers for Schools Kenya (CFSK) ni shirika lisilo la kiserikali linalohusika na ukarabati wa kompyuta iliyoko kiasi cha kilomita 30 nje ya jiji la Nairobi, Kenya, kwenye eneo la viwanda liitwalo Semco Business Park.

Shirika hili lilianzishwa mnamo mwaka 2002 kwa madhumuni ya kukabiliana na ongezeko la kuingizwa kwa kiasi kikubwa vifaa vikuukuu vya kielektroniki. Serikali ya Kenya imelipa mamlaka shirika hilo kukarabati kompyuta. Seth Munyambo, ambaye ni meneja miradi wa shirika hilo, anasema kwamba kinachotokea sasa ni kwamba katika nchi zilizoendelea watu huvitupa vifaa vya elektroniki vilivyozeeka, ambavyo huokotwa na kuletwa barani Afrika kama msaada. Lakini tatizo ni kwamba watu wanakubali misaada hiyo ya vifaa ambavyo vimezeeka na haviwezi kutumika, kwa sababu hakuna kigezo kinachowangoza juu ya kipi wanaweza kukikubali.

Kenya, kama zilivyo nchi nyingi barani Afrika, haina sera na mikakati ya kupambana na hali hiyo. Kwa hivyo, wanawake na watoto, kwa kiasi kikubwa, wanaingia katika hatari ya kukabiliwa na madhara ya kiafya yanayotokana na mabaki ya vifaa hivyo vya elektroniki. Fiona Musana kutoka Shirika la Greenpeace la Afrika Kusini anasema kwamba, ni kawaida kuwaona watoto wadogo wakiwa wanachezea na kubomoa seti la televisheni zilizoharibika, simu za mkononi na vifaa vingine vya kielektroniki, ambavyo vimetupwa barani Afrika.

"Tutashuhudia ongezeko la madhara ya kimazingira na afya za watu masikini wanaoishi katika bara hili."

Munyombo anasema mradi huo ni mchango wa serikali ya Kenya katika kukabiliana na tatizo hilo.

"Ni lazima tuwe na viwango na kwamba kila mmoja katika sekta hii afahamu kuwa, hawezi kuingiza vifaa vya teknolojia ya habari na mawasiliano, ambavyo havifikii viwango hivi."

Lakini hatua zinapasa pia kuchukuliwa na nchi ambako vifaa hivi vinatoka. Kwa mfano, Umoja wa Ulaya umezuia usafirishaji nje wa vifaa hivyo vilivyochoka, hatua mabayo, hata hivyo inakabiliwa na changamoto kubwa kwani wasafirishaji wamekuwa wakidanganya kuwa vifaa hivi vinaweza kutumika.

Matthias Kern ambaye ni afisa mwandamizi katika sekretarieti ya Mkataba wa Basel wa UNEP anasema kuwa kupiga marufu pekee hakutotatua tatizo, kutokana na mahitaji makubwa vya vifaa hivyo katika nchi zinazoendelea.

"Siyo tu kwamba vifaa vya elektroniki vilivyochakaa vinatupwa katika nchi za Afrika, bali kuna sekta nzima isiyo rasmi ambayo inaishi kutokana na vifaa hivyo. Wamekuwa wakitoa vipuri kama vile kutoka kwenye kompyuta mbovu na kujipatia fedha kwa kuwauzia watu wanaohusika na kutengeneza vifa mbalimbali."

Nigeria, Ghana na Afrika Kusini ni miongoni mwa nchi zenye kiwango kikubwa cha vifaa hivi. Na kwa mradi huu wa Computers for Schools huko Kenya, nchi hiyo ya Afrika Mashariki inapiga hatua katika kutafuta sulihisho la tatizo hilo.

Mwandishi: Jane Ayeko/Aboubakary Liongo

Mhariri: Josephat Charo