1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Al-Shabbab yaonya dhidi ya msaada wa Israel kwa Kenya

16 Novemba 2011

Kufuatia ziara ya Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga, nchini Israel ambako ameomba msaada wa kupambana na kundi la Al-Shabbab, kundi hilo sasa linadai msaada huo ni kwa makusudi ya "kuwaangamiza Waislamu na dini yao".

https://p.dw.com/p/13BK2
Wanajeshi wa Kenya wakielekea Somalia, Oktoba 2011.
Wanajeshi wa Kenya wakielekea Somalia, Oktoba 2011.Picha: dapd

Kufuatia mgongano wa kiitikadi na kiusalama kati ya Israel na Al-Shabbab, kundi hilo limelichukulia ombi la Kenya kwa Israel kama uchokozi wa makusudi. Mwaka 2002, Al-Shabbab iliiripuwa kwa mabomu hoteli ya kifahari inayomilikiwa na raia wa Israel karibu na Mombasa na kuwaua watu 13. Kundi hilo lilijaribu pia kuitungua ndege ya Israel iliyokuwa ikiruka kwenye anga ya Kenya.

Sasa msemaji wa Al-Shabbab, Sheikh Ali Mohamud Rage, ameionya Kenya kwamba bado inayo fursa ya kuondoa vikosi vyake nchini Somalia, na sio kuomba msaada wa taifa hilo la Kiyahudi.

"Tunaimbia Kenya kwamba ngoma hasa bado haijapigwa, na tayari ni mwezi mzima sasa. Bado unayo fursa ya kurudi ndani ya mpaka wako." Amesema Rage katika kauli inayochukuliwa kama indhari ya mashambulizi zaidi katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi.

Mshikamano dhidi ya "siasa kali"

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin NetanyahuPicha: AP

Juzi Jumatatu (14.11.2011), ofisi ya waziri mkuu wa Kenya ilisema kwamba nchi hiyo imepata uungwaji mkono wa viongozi wa Israel katika kupambana na kile ilichokiita "dalili za siasa kali". Hiyo ni kufuatia ziara ya siku mbili ya Waziri Mkuu Odinga nchini Israel, akitafuta msaada wa kuimarisha nguvu za vikosi vya usalama vya nchi yake.

Taarifa hiyo imesema kuwa Rais Shimon Peres na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu wameahidi kuisaidia Kenya kulinda mipaka yake na Somalia kujenga mshikamano wa mataifa dhidi ya siasa kali, ambao utazijumuisha pamoja nchi za Kenya, Ethiopia, Sudan Kusini na Tanzania. Serikali ya Israel imeyaita mazungumzo ya Odinga na Netanyahu kama hatua ya kuimarisha mahusiano kati yake na mataifa ya Afrika, bila kueleza undani zaidi.

Watoto zaidi wauawa

Mashambulizi ya mabomu ya Al-Shabbab tarehe 4 Oktoba 2011.
Mashambulizi ya mabomu ya Al-Shabbab tarehe 4 Oktoba 2011.Picha: picture alliance/dpa

Katika upande mwengine, Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) limesema watoto 24 wameuawa na wengine 58 kujeruhiwa mwezi uliopita, ikiwa ni idadi kubwa kwa mwaka huu. Taarifa hii ya UNICEF imetolewa jana, mara baada ya bomu kuripuka kwenye kambi ya wakimbizi nchini Kenya na kuuwa watu wawili.

Mwakilishi wa UNICEF nchini Somalia, Sikander Khan, amesema idadi kamili hasa ya watoto waliouawa na kujeruhiwa huenda ikawa kubwa zaidi.

"Maisha ya watoto wa Kisomali yanazidi kuwekwa rehani kwa kuongezeka kwa mgogoro. Kwa mujibu wa sheria za kimataifa, tunazitaka pande zote zinazohusika na mgogoro wa Somalia kuacha mauaji, mateso, kuwapa mafunzo ya kijeshi vijana na ubakaji wa watoto." Amesema Khan.

Vikosi vya Kenya viliingia nchini Somalia katikati ya mwezi uliopita kupambana na Al-Shabbab, ingawa msemaji wa UNICEF, Jaya Murthy, amesema shirika lake halihusishi ongezeko la vurugu dhidi ya watoto kwa kundi lolote.

Al-Shabbab ilichukuwa dhamana ya mashambulizi ya kujitoa muhanga mjini Mogadishu mwezi uliopita ambayo yaliua zaidi ya watu 100.

UNICEF ni moja kati ya mashirika machache ya kimataifa yanayoweza kufanya kazi kwenye eneo la kusini mwa Somalia linalodhibitiwa na Al-Shabbab.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/AP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman