1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ANKARA: Bunge la Uturuki limeanza kupiga kura leo kumchagua rais

20 Agosti 2007
https://p.dw.com/p/CBXJ

Bunge la Uturuki leo limeanza raundi ya kwanza ya kupiga kura kumchagua rais wa nchi hiyo.

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Uturuki, Abdullah Gül, anatarajiwa kushinda, huku akiahidi kuendeleza maelewano kati ya viongozi wanaohasimiana nchini humo kufuatia miezi kadhaa ya mgogoro wa kisaisa.

Bwana Gül ana nafasi kubwa ya kushinda, miezi michache baada ya Waturuki wasio na msimamo mkali wa kidini wakiungwa mkono na jeshi la Uturuki lenye ushawishi mkubwa, kupinga uteuzi wake na chama cha AK kugombea urais.

Gül anatarajiwa kuwashinda wagombea wengine wawili katika raundi ya tatu ya kura itakayofanyika tarehe 28 mwezi huu.

Ushindi katika awamu mbili za mwanzo unahitaji thuluthi mbili za kura zote bungeni, huku raundi ya tatu ikihitaji tu wingi wowote wa kura.

Chama kikuu cha upinzani nchini Uturuki, Republican People´s Party, kimeapa kuugomea uchaguzi huo kikisema bwana Gül, mshirika mkubwa wa waziri mkuu, Recep Tayyip Erdogan, atasaidia kudunisha sheria na kanuni zisizoelemea dini.