1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BAGHDAD: Wanamgambo wa kishia watuhumiwa kuwateka nyara Waingereza watano

30 Mei 2007
https://p.dw.com/p/CBwd

Viongozi wa Irak wanasema wanashuku wanamgambo wa kishia walio na mafungamano na polisi ya Irak walihusika katika utekaji nyara wa raia watano wa Uingereza mjini Baghdad hapo jana.

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Irak, Hoshyar Zebari, amesema mahala pa utekaji nyara huo ni karibu mji wa Sadr na hiyo ina maana kundi la al-Qaeda halingeweza kufanya operesheni hiyo.

Wanajeshi wa Marekani na wa Irak wamevivamia vitongoji vya Baghdad usiku kucha kuwatafuta Waingereza watano waliotekwa nyara hapo jana kutoka kwa jengo la serikali.

Watu waliovalia sare za polisi waliwateka nyara Waingereza hao kutoka kwa kituo cha kompyuta cha wizara ya fedha mjini Baghdad.

Robin Horsfall, afisa wa zamani wa kitengo maalumu cha usalama nchini Uingereza, SAS, amesema, ´Hali ya wafanyakazi wa mikataba wanaokwenda kufanya kazi nchini Irak ni hatari zaidi kuliko wanajeshi walio Irak. Hawana msaada wa usalama wala watu wa kuwasaidia. Mara nyingi hawajui wanaenda kufanya kazi na nani mpaka wafike nchini humo.´

Kampuni ya usalama kutoka Canada iitwayo, GardaWorld, imethibitisha kwamba walinzi wake wanne raia wa Uingereza na mtaalamu mmoja wa kopyuta Muingereza walitekwa nyara katika uvamizi huo wa jana.

Zaidi ya raia 200 wa kigeni na maelfu ya Wairak wametekwa nyara tangu uvamizi wa Irak ulioongozwa na Marekani mnamo mwaka wa 2003. Mateka wa rehani takriban 60 wa kigeni wameuwawa nchini Irak na watu waliokuwa wakiwazuilia.