1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bara la Ulaya latuliza mvutano wake na Marekani

Halima Nyanza14 Desemba 2007

Ulaya imetuliza mvutano wake uliokuwepo na Marekani kuhusiana na malengo ya hali ya hewa kwa mwaka 2020, katika siku ya mwisho ya mkutano wa Bali, hali ambayo inaleta matumaini ya kuanza kwa mjadala kuhusu mkataba mpya.

https://p.dw.com/p/Cbr8
Waziri wa Mazingira wa Ujerumani Sigmar Gabriel.Picha: picture-alliance / dpa

Taarifa hiyo imelezwa na Waziri wa Mazingira wa Ujerumani Sigmar Gabriel ambaye amesema jambo hilo limeleta hali nzuri katika mkutano huo wa Bali, hali inayoonesha kupatikana na mafanikio mwisho wa mkutano huo.

Amesema pande zote zinapaswa kuwa tayari, kutafuta muafaka na kuongeza kuwa, Ulaya, inasisitiza mkutano huo wa Bali unapaswa kutoa mwongozo mzito kwa mwaka 2020 kuhusiana na gesi chafu inayotolewa licha ya upinzani kutoka Marekani.

Kwa upande wake Mshauri wa Serikali ya Ujerumani katika mkutano mkuu wa Hali ya Hewa unaofanyika Katika kisicha Bali, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Uchunguzi wa Hali ya Hewa mjini Potsdam, Ujerumani, Hans- Joachim Schellnhuber alielezea kuwepo kwa ugumu katika kupatikana kwa makubaliano katika mkutano huo kutokana na Marekani, na baadhi ya nchi kukataa kukubali masharti yanayotakiwa katika mkutano huo.

’’Yaani, nchi sasa zimetambua kwamba tunazungumzia mambo mazito, Na ahadi zinazotolewa sasa zinatakiwa kweli zitimizwe na sio kama ilivyokuwa mwaka 1997, ambapo mkataba wa Kyoto ulipopitishwa. Wakati ule hakukuwa na uhakika wa makadirio ya wanasayansi kwamba hali ya hewa itakuwa tatizo kubwa siku zinazokuja, na ni kweli kama tunavyoona hii leo’’.

Mazungumzo hayo kuhusiana na mabadiliko ya Hali ya Hewa ambayo yalianza Desemba tatu yana lengo la kufikia makubaliano ya kuzindua majadiliano ya miaka miwili ili kuweza kusainiwa kwa mkataba mpya utakaochukua nafasi wa mkataba wa Kyoto, ambao unamalizika mwaka 2012.

Umoja wa Mataifa unataka mpango huo mpya kuhusisha mataifa yote, yakiongozwa na Marekani, nchi ambayo inaongoza kwa kutoka gesi chafu duniani zikiwemo pia, China na India.

Awali Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki- Moon alitahadharisha uwezekano wa kutofanikiwa kwa mkutano huo, lakini aliweka matumaini ya kufikiwa makubaliano.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kesho Jumamosi anatarajiwa kuzungumza na wanahabari kuhusiana na mkutano huo.

Wanaharakati mbalimbali waliohudhuria mkutano huo walionekana nje ya jengo lililokuwa likifanyika mkutano, ambapo walikuwa wakiwasilisha ujumbe wao, kwa wajumbe wa mkutano huo kwamba dunia tayari imeshaanza kuonja adha ya mabadiliko ya hali ya hewa.

Katika mkutano huo wa Bali wajumbe walikubaliana pia uchukuliwaji hatua katika kupunguza kutowekwa kwa misitu, kutokana na kwamba misitu ndiyo inayochukua hewa chafu inayotolewa.

Makubaliano hayo yameelezwa kuwa ni mojawapo ya mafanikio ya mkutano huo.

Mapema jana katika mkutano huo kulitokea mvutano kati ya nchi za Umoja wa Ulaya na Marekani ambapo kila upande ulikuwa ukimlaumu mwenzake kukwamisha uzinduzi wa mazungumzo hayo.

Kutokana na hali hiyo Umoja wa Ulaya ulitishia kugomea mazungumzo ya Marekani kuhusiana na hali ya hewa yanayotarajiwa kufanyika katika visiwa vya Hawaii mwezi ujao endapo mtihani huo wa Bali hautafanikiwa.