1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza jipya la mawaziri nchini Ujerumani

Oumilkher Hamidou26 Oktoba 2009

Washirika wepya wamekamilisha mazungumzo ya kuunda serikali mjini Berlin

https://p.dw.com/p/KFOn
Washirika katika serikali mpya ya muungano:kutoka kushoto,Horst Seehofer wa CSU,Guido Westerwelle wa FDP na kansela Angela Merkel wa chama cha CDUPicha: AP

"Nafuu za kodi ya mapato kwaajili ya familia na wajasiria mali,"kinga" kwa waajiriwa na sura mpya katika baraza jipya la mawaziri"-serikali mpya ya muungano wa vyama vya CDU/CSU na waliberali wa FDP,au kama unavyoitwa muungano wa nyeusi na manjano,inafafanua malengo yake na kuwajulisha mawaziri wake.

Hakuna kinachowakasirisha zaidi washirika wepya serikalini kama dhana wanazotupiwa eti watasababisha kuondoka patupu wasiojimudu kifedha.Atakaekua naibu kansela,mliberali Guido Westerwelle amesema walipokua wakifafanua mkataba wa muungano mjini Berlin:

"Wote wale ambao kabla ya uchaguzi walihoji kwamba muungano wa nyeusi na manjano utakua mfano wa hatari ya kijamii,mkataba huu wa muungano unawasuta."

Muungano wa nyeusi na manjano haujaishia tuu kutangaza nafuu kwa wakosa ajira wa muda mrefu-watakaojionea kiwango chao cha"raslimali " kikizidishwa,bali pia muungano huo umetangaza dhamiri za kuimarisha "kinga" kwa waajiriwa -kama alivyosisitiza kanseka wa zamani na mpya Angela Merkel.

"Serikali mpya inatekeleza ahadi ilizotoa na hali hiyo inaonekana wazi wazi katika mkataba wa muungano.Hatupandishi kodi,tunalenga ukuaji wa kiuchumi ,tunawapunguzia mzigo raia wake kwa waume."

Kwa familia zenye watoto,warithi na wajasiria mali,kuanzia mwakani watapunguziwa mzigo wenye thamani ya zaidi ya yuro bilioni 20-lakini yuro bilioni 14 kati ya hizo zinatokana na makubaliano yaliyofikiwa na serikali iliyotangulia.

Zaidi ya hayo serikali inapanga kujaza makasha ya bima ya wasiokua na ajira na bima ya afya.Kwakua Ujerumani inakadiria kuwa na nakisi iliyokithiri -yuro bilioni 76 kwa mwaka 2010,serikali mpya ya muungano ilifikiria kutoa fedha hizo kutoka bajeti ya siri-lakini fikra hiyo iliachiliwa mbali kutokana na lawama zilizofuatia pamoja na hoja kwamba pengine fikra kama hiyo haiambatani na muongozo wa katiba.

Wizara ya fedha katika baraza jipya la mawaziri la kanselka Angela Merkel itaongozwa na aliyekua waziri wa mambo ya ndani Wolfgang Schäuble.Hata upande wa upinzani umesifu uamuzi huo kwasababu mfuasi huyo wa chama cha Christian Democratic Union ni mwanasiasa anaefaa na mwenye moyo wa kupitisha maamuzi hata kama watu wataudhika.

Lawama kali za mashirika ya huduma za jamii zilisikika pale serikali mpya ilipodokeza azma ya kugharimia vyengine kabisa bima ya afya inayodhibitiwa na serikali.Michango ilikua isifungamanishwe tena na kiwango cha mshahara mfanyakazi anaopokea,badala yake ilikua pawepo kiwango jumla na sawa kwa wote.Pekee wenye kupokea mishahara duni ndio waliokua wapatiwe msaada wa serikali.

Philipp Rösler Das neue Kabinett
Waziri mpya wa afya,Philipp RößlerPicha: picture-alliance / dpa

Kazi ngumu katika wizara ya afya inamsubiri mwanasiasa kijana,mliberali Philip Rösler.Kijana huyo aliyezaliwa mwaka 1973 nchini Vietnam,alipokua mdogo alilelewa na familia ya kijerumani na kusomea udaktari nchini Ujerumani.

Wizara ya mambo ya nchi za nje anashikilia mwenyewe mwenyekiti wa chama cha FDP Guido Westerwelle anaesema,siasa ya nje ya Ujerumani sio tuu itaendelea kama ilivyo,bali pia Ujerumani itaendelea na juhudi za kutaka itakaswe na silaha za kinuklea."

Waliberali wanadhibiti wizara tano,ikiwa ni pamoja na wizara ya misaada ya maendeleo.

Waziri wa zamani wa uchumi Karl-Theodor zu Guttenberg,amechaguliwa kua waziri wa ulinzi.Kwakua babu yake baake alikua miongoni mwa walioandaa njama iliyoshindwa ya kutaka kumuuwa Hitler,Karl Theodor zu Guttenberg anaangaliwa kua ni mtu anaefaa kudhibiti wizara ya ulinzi.

Mwandishi:Bernd Gräßler/Hamidou Oummilkheir

Mhariri: Abdul-Rahman